• HABARI MPYA

  Saturday, March 28, 2009

  AMIR MHANDO WIKI HII; NG'OMBE ANAYECHELEWESHA MSAFARA...


  (KULIA NI MWANDISHI WA MAKALA HAYA, AMIR MHANDO)
  WIKI hii naamini mashabiki wa Yanga ya Dar es Salaam watakuwa na furaha zaidi baada ya timu yao ya soka kutetea ubingwa wake wa Tanzania Bara kwa mwaka 2008/2009. Yanga imetwaa ubingwa huo kwa mwaka wa pili mfululizo, baada ya kuifunga Toto African mabao 2-1, mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza. Kutokana na ushindi wa mchezo huo uliofanyika Jumanne, Yanga imefikisha pointi 46, ambazo hakuna timu nyingine yoyote inaweza kuzifikia. Nawapongeza wachezaji, viongozi na makocha wa Yanga kwa jitihada zao hadi kufanikiwa kutwaa tena kombe hilo, hivyo inaonyesha jinsi walivyokuwa na mshikamano na nia thabiti ya kuwapa raha mashabiki wao. Lakini kabla ya mechi ya Yanga haijachezwa, timu hiyo ilikuwa na pointi 45 na ilielezwa ilikuwa ikihitaji sare ya aina yoyote ifikishe pointi 46, ambazo zisingefikiwa na timu nyingine 11 zinazoshiriki ligi hiyo. Hata hivyo, siku moja kabla ya mchezo huo ziliibuka taarifa kuwa Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF), liliipoka Yanga pointi mbili ilizopewa katika mchezo dhidi ya Polisi Morogoro katika duru la kwanza, ambao ulimalizika kwa timu hizo kutoka sare. TFF iliipa ushindi Yanga bila kukata rufani, baada ya kujiridhisha kuwa Polisi ilimchezesha Tafaa Daud aliyekuwa na kadi tatu za njano, kabla ya baadaye kujiridhisha kuwa uamuzi wa kuipa Yanga ushindi haukuwa sahihi. Kutokana na uamuzi huo wa TFF, Yanga ikajikuta inabaki na pointi 43, hivyo kwa ushindi wa Jumanne imefikisha pointi 46, ambapo Kagera Sugar na Simba zenye pointi 27 na michezo mitano mkononi, kama zikishinda michezo yao iliyobaki zitafikisha pointi 42. Ukiachana na suala la ubingwa wa Yanga, kuna jambo ambalo binafsi naona ni doa na halipaswi kujirudia siku za usoni, maana linapoteza maana halisi ya ligi. Kupeana pointi za mezani! Dunia ya sasa mambo ya kupeana pointi za bure hayapewi nafasi, kwanza sidhani kama yanahitajika, ili iweje? Hata kama timu itapokwa ushindi, lakini zile pointi haipewi timu nyingine, maana si zake. Hilo ndilo lililotokea kwa Yanga na Polisi Morogoro, timu hizi zilitoka sare katika mchezo wa duru la kwanza, lakini katika hali isiyo ya kawaida, waungwana hawa wakajivika jukumu la ulalamikaji, kisha wakawa waendesha mashitaka na mwishoni mahakimu. Wakatumia kanuni zao katika Kamati ya Mashindano iliyopita wakaiondolea pointi moja Polisi Morogoro, wakaiongezea pointi mbili Yanga, ambayo hata ilikuwa haina habari. Kwa kiasi fulani ilipoozesha mambo, Yanga iliyokuwa na pointi nyingi ikaongezewa nyingine, ikamaliza duru la kwanza ikiwa na hazina ya pointi. Sisi tunaopenda kuhoji mambo tukasema huu si uungwana na ni kupoozesha mashindano. Hakukuwa na sababu. Lakini ikapita, ikawa asubuhi, mchana, jioni, siku ikaisha, wiki mwezi na kisha miezi karibu minne sasa, inakuja taarifa nyingine kuwa Yanga imenyang'anywa zile pointi na TFF. Hii si mara ya kwanza kutokea matatizo kama haya ya utata wa pointi katika hatua za mwisho za michezo, wadau wanakumbuka mwaka jana wakati ligi ikiwa inakaribia kumalizika, pia mgogoro kama huu ulijitokeza. Simba ya Dar es Salaam ilipokwa pointi tatu na Kamati ya Mashindano ya TFF kwa madai ilimchezesha Juma Nyosso aliyekuwa amefungiwa na shirikisho hilo kucheza soka kwa miezi mitatu Novemba mwaka juzi, akidaiwa kumpiga kiwiko mchezaji wa Toto African katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, wakati huo akichezea Ashanti United. Lakini mchezaji huyo alisajiliwa Simba katika dirisha dogo la usajili, siku chache baada ya kuanza kutumikia adhabu yake. Simba nao bila kukumbuka kwamba kijana huyu anatumikia adhabu, wakamtumia katika mchezo wa ligi dhidi ya Coastal. Binafsi, nayatazama matukio haya na mfumo ambao TFF inauendesha katika kutekeleza majukumu yake ya kila siku. Nauita mfumo ng'ombe. Ndio huu ni mfumo ng'ombe ambao hauwezi kusaidia soka letu. Waliopata kuchunga ng'ombe wanajua ninaposema mfumo ng'ombe namaanisha nini. Yaani ng'ombe wawapo katika msafara unakuta anaychelewesha yupo mbele, lakini ajabu viboko anapigwa wa nyuma. Eti ndio wachanganye mwendo! Kwa suala kama lile la Nyoso je alipewa barua ya kufungiwa? Barua mathalani walipewa viongozi wa klabu yake aliyokuwa akichezea yaani Ashanti. Je, hawa viongozi wa Ashanti walimjulisha kijana wao kuhusiana na adhabu hiyo? Au walitegemea labda atasoma katika magazeti? Maana ndiyo njia rahisi ya kupashana habari katika mambo ya soka. Au katika mazingira ya kawaida, je, Ashanti waliwajulisha Simba kuhusiana na adhabu hiyo? Jibu ni hapana si kazi yao, kufanya hivyo bali ya TFF. Kimsingi ukitaka utazame kuanzia suala la Nyoso hadi la Tafaa Daud utagundua mambo mengi sana, kwamba TFF haina utaratibu mzuri kwa mchezaji anapofungiwa kuweka kumbukumbu ili kuzijulisha klabu kama yanavyofanya mashirikisho mengine makubwa ya soka ulimwenguni kama FIFA, CAF na UEFA. Laiti kama TFF ingekuwa na utaratibu mzuri wa kuzipa taarifa klabu, nina hakika mambo kama haya yasingetokea. Mwaka 2006 Simba iliingia katika matatizo kama haya baada ya kudaiwa kumchezesha Mussa Hassan 'Mgosi' aliyekuwa na kadi tatu za njano katika mchezo dhidi ya Kagera Sugar. Tukubali katika hili Kamati ya Mashindano ya TFF inastahili lawama, lazima ijipange upya ili kuhakikisha dosari kama hizi hazijitokezi. Wasilazimishe kuwa mashuhuda mahali walipopaswa kuwa watendaji na wala tusilazimishwe kushangilia tulipopaswa kuzomea, kwani kwa mtindo huu wa kupeana pointi au kunyang'anyana haturekibishi soka letu. Mengi yataibuka hivi sasa hasa wakati huu ambapo timu zinagombea zisishuke daraja, sasa ni vyema yakaepukwa mambo ambayo yanaweza kuzipunguzia nguvu baadhi ya timu au kuziongezea nguvu nyingine.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: AMIR MHANDO WIKI HII; NG'OMBE ANAYECHELEWESHA MSAFARA... Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top