• HABARI MPYA

    Friday, March 20, 2009

    MINZIRO AMKINGIA KIFUA MAXIMO

    Minziro wa nne kutoka kushoto kwenye kikosi cha Yanga mwaka 1987


    KOCHA wa timu ya soka ya Moro United ya Morogoro, Fred Felix Minziro amesema kwamba soka ya Tanzania ingerejea chumba cha wagonjwa mahututi (ICU) iwapo Marcio Maximo asingeongeza mkataba wa kuendelea kuinoa timu ya taifa, Taifa Stars.
    “Angeondoka Maximo hapa, hii timu ya taifa haiwezi kuwa hivi unavyoiona hivi sasa, huyu jamaa kafanya kazi kubwa sana, lazima tukubali bwana,”alisema Minziro alipozungumza na DIMBA juzi mjini Dar es Salaam.
    Minziro amempongeza rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Leodegar Tenga na kamati yake ya Utendaji kwa kumuongezea mkataba mwalimu huyo.
    Kocha huyo kutoka Brazil alianza kuinoa Stars Julai 2006 na hadi anasaini mkataba mpya, alikuwa amekwishaiongoza timu katika mechi 47, kati ya hizo ameshinda mechi 21, sare 14 na kufungwa 12.
    Kati ya mechi hizo, zimo za kuwania tiketi ya fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika nchini Ghana mwaka 2008, fainali za Kombe la Dunia mwaka 2010 nchini Afrika Kusini na fainali za Michuano ya ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN) zilizofanyika Ivory Coast mwezi uliopita.
    Kuelekea Ghana, Tanzania ilikuwa kundi moja na Senegal, Burkina Fasso na Msumbiji na mwisho wa siku Simba wa Teranga ndio waliokata tiketi ya kwenda kwenye fainali hizo wakati Taifa Stars ilishika nafasi ya tatu, Mambas ilikuwa ya pili na Burkinabe walishika mkia.
    Chini ya Maximo Stars ilianza kuilaza Burkina 2-1 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kabla ya kwenda kulazimisha sare ya bila kufungana na Msumbiji mjini Maputo, baadaye kufungwa 4-0 na Senegal.
    Mzunguko wa pili, Stars ilianza kwa kulazimishwa sare ya 1-1 nyumbani na Senegal, kabla ya kwenda kuifunga Burkina Fasso nyumbani kwake 1-0 na mchezo wa mwisho ilifungwa 1-0 nyumbani Msumbiji.
    Kuwania tiketi ya Afrika Kusini, Stars ilianza kwa kulazimishwa sare ya 1-1 na Mauritius nyumbani, kabla ya kufungwa 1-0 na Cape Verde ugenini wakati mchezo wa tatu, ililazimishwa sare ya bila kufungana na Cameroon nyumbani.
    Mchezo wa nne Stars ilifungwa 2-1 na Cameroon mjini Younde, kabla ya kukusanya pointi sita katika mechi zake mbili za mwisho, ikianza kuifunga Mauritius 4-1 kwake na baadaye kurejea nyumbani kuichapa Cape Verde 3-1.
    Mtihani wa tatu kwa Maximo ulikuwa ni kuwania tiketi ya michuani mipya, CHAN na ilianza kwa kufungwa 1-0 na Kenya mjini Nairobi, kabla ya kuibuka na ushindi wa 2-0 nyumbani, Dar es Salaam hivyo kusonga mbele kwa ushindi wa jumla wa 2-1.
    Katika hatua iliyofuata, Tanzania ilianza kwa kuifunga Uganda 2-0 Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza na kwenye marudiano mjini Kampala, Uganda ililazimisha sare ya 1-1 na kusonga mbele.
    Maximo aliiwezesha Stars kuweka rekodi ya kuwa miongoni mwa mataifa nane ya kwanza kucheza CHAN, baada ya kuifunga Sudan jumla ya mabao 5-2, ikianza kushinda 3-1 nyumbani na baadaye 2-1 ugenini.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MINZIRO AMKINGIA KIFUA MAXIMO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top