• HABARI MPYA

    Tuesday, March 17, 2009

    SIMBA YAFUFUA MATUMAINI YA KUCHEZA AFRIKA 2010


    LIGI Kuu ya Vodacom, raundi ya pili imeendelea tena jana kwa Simba kuilaza Moro United mabao 2-1 katika mchezo mkali uliofanyika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam jijini Dar es Salaam.
    Mabao hayo, likiwamo la penalti la Mussa Hassan Mgosi , dakika ya 40 na jingine la Haruna Moshi 'Boban', dakika ya 76 yaliibeba timu yao ambayo awali ilikuwa na kosa kosa nyingi kama ilivyo kwa wapinzani wao.
    Bao la kufutia machozi la vijana hao wa Fred Felix Minziro liliwekwa kimiani, dakika ya 86 na Seleman Kibuta aliyetengewa mpira na Patrick Mangungulu.
    Penalti hiyo ya Simba ilitokana na Amri Kiemba wa Moro United kumwangusha Henry Joseph katika eneo la hatari.
    Hata hivyo, mkwaju huo ulirudiwa kupigwa baada ya beki Juma Nyosso kuingia eneo la 18 kabla ya kupigwa kwa penalti hiyo.
    Katika mchezo wa jana, Samuel Ngassa alikuwa wa kwanza kuikosesha timu yake bao, dakika ya tisa ya mchezo baada ya kuwatoka mabeki wa Simba na kuachia shuti ambalo lilipaa mita chache nje ya lango la wapinzani wao.
    Wekundu wa Msimbazi walijibu muda mfupi baadaye kupitia kwa kiungo Henry Joseph ambaye pia alikosa bao kutokana na mpira wa adhabu ndogo wa Juma Jabu, kichwa chake kikatoka nje.
    Nahodha wao, Nico Nyagawa, alikosa bao dakika ya 22 ya mchezo baada ya kumegewa pasi ya Mgosi.
    Kosa kosa hizo ziliendelea kwa Moro United ambao kupitia kwa Pius Kisambale aliyewahi kuichezea Simba, alikosa bao dakika ya 27 kutokana na krosi safi ya Nizar Khalfan. Kipa wa Simba, Deo Mushi 'Dida' aliudaka mpira huo.
    Dakika ya 68, kipindi cha pili, Moro walimzonga mwamuzi wakidai kunyimwa penalti ya wazi baada ya beki wa Simba, Meshack Abel kumwangusha Kudra Omari katika eneo la hatari.
    Kocha wa Simba, Patrick alieleza kuridhishwa na matokeo ya mechi hiyo akieleza kuwa mazoezi dhidi ya Vancouver Whitecaps yamesadia, ingawa alikiri kuwa mechi ilikuwa ngumu na ushindani.
    Juzi, Azam FC na Mtibwa Sugar zilitoka sare ya bao 1-1 katika mchezo mwingine wa ligi hiyo ambayo ilirejea wiki iliyopita kwa JKT Ruvu kuiadhibu Villa Squad mabao 5-1.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SIMBA YAFUFUA MATUMAINI YA KUCHEZA AFRIKA 2010 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top