• HABARI MPYA

  Monday, March 16, 2009

  MAXIMO AWAPASHA WANAOCHONGA...


  KOCHA wa Taifa Stars, Marcio Maximo amesema kamwe hatovunja taratibu zinazoongoza taaluma yake kwa kuogopa kelele za mashabiki ambao kila mmoja anaongozwa na mapenzi yake binafsi.
  Maximo alitoa kauli hiyo katika mahojiano maalumu na Mwananchi kuhusiana na vitendo vya hivi karibuni vilivyofanywa na mashabiki wa klabu za Yanga na Simba kumzomea wakati timu zao zilipokuwa zikipambana dhidi ya mabingwa wa Amerika ya Kaskazini, Vancouver White Caps mechi zilizofanyika kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
  Katika mechi hizo Mashabiki wa Yanga walionekana kulitaja jina la Maximo kila wakati ambao kiungo wa timu hiyo Athumani Iddi 'Chuji' alipokuwa na mpira kadhalika hivyo hivyo mashabiki wa Simba walionekana kupiga kelele wakilitaja jina la Mbrazil huyo wakati mchezaji Haruna Moshi'Boban' alipokuwa na mpira.
  Maximo alisema kamwe hata siku moja hawezi kuogopa kelele za mashabiki ambao kimsingi kila mmoja ana mapenzi yake kwa mchezaji fulani kwani kwa kufanya hivyo amevunja misingi ya taaluma yake.
  "Nakwambia bwana mashabiki wanalipa kiingilio kwa ajili ya kuangalia mechi, lakini pia kila mmoja ana mapenzi yake kwa mchezaji fulani hivyo huwezi kuwazuia kuongea kile wanachofikiria kwani wana uhuru wa kufanya hivyo, isipokuwa wewe kama kocha uliyesomea kazi yako unatakiwa kusimama kama misingi ya taaluma yako inavyotaka,"alisema Maximo.
  "Napenda kukwambia kwamba nimeanza kufundisha soka nikiwa kijana sana na mpaka sasa nimekwisha kuwa kocha mkuu wa mataifa manne, lakini pia nimekaa katika nchi saba tofauti nikifundisha soka na kukumbana na matatizo mengi yakiwemo hayo ya mashabiki na kuyakabili, hivyo sioni sababu ya kutetereka kwa sasa.
  Aidha Maximo ambaye hivi karibuni aliteua chipukizi wengi katika kikosi chake aliwakumbusha wapenzi wa soka hapa nchini kuwa na uvumilivu na kutambua kuwa Tanzania ndiyo kwanza imeanza, hivyo si vizuri kujilinganisha na nchi kama Nigeria, Cameroon na nyingine ambao zimepata mafanikio baada ya kuwekeza miaka mingi.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MAXIMO AWAPASHA WANAOCHONGA... Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top