• HABARI MPYA

  Friday, March 20, 2009

  PAN WAITISHA UCHAGUZI


  WANACHAMA wa timu ya soka ya Pan Africa ya Dar es Salaam, wametakiwa kujitokeza kwa wingi kuchukua fomu za kugombea nafasi za uongozi ili watoe mchango wao katika kuiletea maendeleo timu hiyo.
  Akizungumza jijini Dar es Salaam juzi, Katibu Mkuu wa timu hiyo, Saad Mateo, alisema kuwa zoezi la uchukuaji fomu limeanza toka Machi 17 na mwisho wa kurudisha fomu ni Machi 30.
  “Tunahitaji wanachama wenye nia na moyo wa kuendesha soka ambao watakuwa tayari kufufua na kurudisha heshima ya Pan Africa katika kama za zamani,” alisema.
  Nafasi zinazowaniwa katika uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika Aprili 12 mwaka huu, ni Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti, Katibu Mkuu, Mweka Hazina, Katibu Mkuu Msaidizi na Wajumbe.
  Hata hivyo, Mathew ameweka wazi nia yake ya kutetea nafasi yake ya Katibu, ambako alisema kuwa anahitaji kurejea tena madarakani ili kukamilisha malengo yake ya kuiletea maendeleo timu hiyo.
  Miongoni mwa malengo hayo ni pamoja na kuhakikisha timu inakuwa na vitega uchumi vyake na kuwa na gazeti la timu na kuhakikisha timu inakuwa na wafadhili wa kudumu. (PICHANI KUSHOTO NI MCHEZAJI WA ZAMANI NA MWANACHAMA WA PAN, LEODEGAR TENGA)


  Mtibwa yaitishia nyau Simba

  TIMU ya Mtibwa Sugar ya Turiani, Morogoro, imewaonya Simba kuwa wasitegemee urahisi kwenye mechi yao itakayochezwa Jumapili, katika Uwanja wa Jamhuri, Morogoro.
  Kauli hiyo ilitolewa na kipa wa Mtibwa, Shaaban Kado, ambaye alisema kwamba wamejipanga vyema kwa ajili ya kushinda mechi hiyo.
  Mechi hiyo inategemewa kutoa nafasi kubwa kwa klabu hizo zinazowania nafasi ya pili, baada ya kushindwa kunyakua taji hilo baada ya kuachwa mbali na Bingwa mtetezi wa ligi hiyo, Yanga.
  Ukiacha mechi ya jana kati ya Yanga na Polisi Morogoro, klabu hiyo iliyokung’utwa mabao 3-0 na Al Ahly ya Misri, inaongoza katika msimamo huo kwa pointi 41, wakati Simba inashika nafasi ya pili kwa pointi 27, huku Mtibwa ikiwa na pointi 22.
  Akifafanua zaidi, Kado alisema kwamba wanatambua umuhimu wa mechi hiyo na kwamba wamejiandaa ili wajiweke kwenye mazingira mazuri ya kupata nafasi ya pili.
  Alisema kitendo cha kukubali kufungwa na Simba, kitawarudisha nyuma katika mbio zao za kuwania nafasi ya kucheza michuano mikubwa, hususan ya Kombe la Shirikisho.
  “Kuna kila sababu ya kushinda mechi yetu na Simba, ukizingatia kwamba na sisi tunataka kutangaza timu yetu nje ya nchi katika michuano mikubwa Barani Afrika,” alisema.
  “Wote tupo katika mazingira mazuri, na naamini Simba hawataweza kutufunga, ingawa na wao wamepania vikali katika mchezo huo utakaochezwa katika uwanja wetu wa nyumbani.”
  Hivi karibuni, Mtibwa iliweza kunyakua Kombe la Tusker kwa mara ya kwanza, huku ikiziacha klabu kubwa za Simba na Yanga zikishindwa kutamba katika patashika hizo zilizoshirikisha timu mbili kutoka nje ya nchi.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: PAN WAITISHA UCHAGUZI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top