• HABARI MPYA

  Jumanne, Machi 10, 2009

  PHIRI ASEMA SIMBA SASA IKO KAMILI  KOCHA wa klabu ya Simba ya Dar es Salaam, Patrick Phiri (pichani juu) amesema mapumziko ya zaidi ya mwezi mmoja kwenye Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, yamempa fursa ya kujipanga vizuri ili kumalizia mechi zilizosalia, akiwa na matumaini makubwa ya kupata nafasi ya kuiwakilisha nchi kwenye michuano ya Afrika mwakani.
  Akizungumza na DIMBA juzi mjini Dar es Salaam, Phiri alisema anashukuru wachezaji wake waliokuwa majeruhi sasa wamepona wote na wale ambao hawakuwa fiti, sasa wameimarika, hivyo anaamini atakata kiu ya wana Simba.
  Aliwataja wachezaji ambao walikuwa majeruhi na sasa wako fiti kabisa ni kiungo Mohamed Simba Banka na mshambuliaji Moses Godwin Mwazembe ambaye aliwahi kuitwa na Marcio Maximo kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Desemba mwaka jana lakini akatemwa kutokana na maumivu yake.
  Aidha, kocha huyo alisifia hali ya nidhamu kwa wachezaji wake hasa wale chipukizi, kwamba inamtia moyo na kama wataendelea hivyo, anaamini kabisa mambo yatakuwa safi katika mechi zilizosalia za ligi hiyo.
  “Tuna vita kubwa kuhakikisha msimu unamalizika tukiwa katika nafasi ya pili, hilo ndio lengo kuu, nashukuru kampeni zinaendelea vizuri,”alisema kocha huyo raia wa Zambia.
  Phiri alisema mchezo wa kujipima nguvu dhidi ya Vancouver Whites Caps ya Canada, ndio utatoa picha ya SImba ilivyoimarika kwa sasa na amewataka mashabiki wa timu hiyo, kujitokeza kwa wingi uwanjani kesho kushuhudia mechi hiyo.
  Kuhusu wapinzani wao hao wa kesho, Phiri alisema ni wazuri ndio maana Yanga walipigana kwa nguvu zao zote kupata mabao matatu, hivyo anaamini kwake pia utakuwa mchezo mzuri wa kuipima Simba.
  “Hawa (Whitecaps) ni wazuri, kilichowaathiri ni hali ya hewa tu, kwao ni baridi na hapa ni joto, lakini ni timu nzuri kujipima nayo,”alisema mtaalamu huyo aliyeiongoza Zambia katika Kombe la Mataifa ya Afrika (CAN) nchini Ghana mwaka juzi.
  Kikosi cha Simba kwa sasa kinaundwa na makipa Amani Simba, Deo Munishi ‘Dida’, Ally Mustafa ‘Barthez’, mabeki Salum Kanoni, Anthony Matangalu,Juma Jabu, David Naftali, Meshack Abel, Kelvin Yondan, Ramadhan Wasso, viungo Henry Joseph, Nico Nyagawa, Juma Said Nyoso, Ramadhani Chombo ‘Redondo’, Nassoro Masoud ‘Choro’, Banka, Ulimboka Mwakingwe, Mussa Hassan Mgosi, Jabir Aziz na Adam Kingwande.
  Washambuliaji ni Mwazembe, Mohamed Kijuso, Haruna Moshi ‘Boban’ na Wanigeria, Emeh Izichukwu na Orji Obinna.
  Wachezaji wengine waliosajiliwa na Simba msimu huu, beki Victor Costa aliyetimkia Botswana, Edwin Mukenya alifukuzwa kwa utovu wa nidhamu, Emmanuel Gabriel aliuzwa Uarabuni na George Nyanda amebanwa na masomo katika Chuo cha Biashara (CBE) Dodoma.
  Simba inatarajiwa kuanza tena kampeni zake za kuwania nafasi ya pili Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Machi 14, mwaka huu kwa kumenyana na Moro United mjini Dar es Salaam.
  Wekundu hao wa Msimbazi, wanaoshika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu, wanahitaji kushinda mechi zao zote saba za Ligi Kuu zilizobaki, ili kutimiza pointi 45 na kufufua matumaini ya kupata nafasi ya pili. Kwa sasa, nafasi ya pili inashikiliwa na kagera Sugar ya Bukoba yenye pointi 26, ikiwa imebakiza pia mechi saba.
  Simba inashika nafasi ya tatu kwenye ligi hiyo, ikiwa na pointi 24, Kagera Sugar inayoshika nafasi ya pili ina pointi 26.
  Tayari watani wao wa jadi, Yanga wameukaribia ubingwa wa ligi hiyo, wakiwa wana pointi 42 na wanahitaji pointi nne tu katika mechi zao saba, ili kutangaza ubingwa mapema.
  Mechi ambazo Simba imebakiza ni dhidi ya Moro United, Mtibwa Sugar mjini Morogoro Machi 22, Azam Machi 29, Kagera Aprili 5 mjini Bukoba, Toto Afrika Aprili 12, Yanga Aprili 19 au 23 na Polisi mjini Dodoma Aprili 26 ambao ndio utakuwa mchezo wa mwisho.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: PHIRI ASEMA SIMBA SASA IKO KAMILI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top