• HABARI MPYA

  Tuesday, March 10, 2009

  MATUMLA AMFUATA SMITH UINGEREZA


  BONDIA Rashid 'Snake Boy' Matumla(PICHANI), aliondoka jana jioni mjini Dar es Salaam kwenda London, Uingereza kwa ajili ya pambano lake la kuwania taji la Chama cha Ngumi Duniani (WBA) International, uzito wa Super Middle dhidi ya mwenyeji, Paul Smith, likalaofanyika Jumamosi wiki hii, ukumbi wa MEN Arena.
  “Ninaondoka leo jioni, niko fiti kabisa, nawaahidi Watanzania wajiandae kunipokea nikiwa nina mkanda wa ubingwa wa WBA,”alisema Rashid bingwa wa zamani wa WBU, uzito wa Light Middle, alipozungumza na DIMBA jana.
  Matumla, ambaye mwezi uliopita alimshukia Francis Cheka kwenye uzito wa Middle katika pambano alilopoteza kwa pointi, atazipiga kwa raundi 12, hilo likiwa pambano la utangulizi kabla ya Amir Khan kuzipiga na Barrera.
  Smith naye amelazimika kurejea kwenye uzito wa Super-Middle ili kutimiza dhamira yake ya kutwaa taji na amekuwa akitamba kwamba amejifua vikali kuhakikisha anatwaa taji hilo la dunia.
  Matumla anayekumbukwa kwa rekodi yake ya kupigana mapambano 29 mfululizo bila kupigwa hadi anatwaa ubingwa wa WBU, atapanda ulingoni kwa mara ya 50 siku hiyo akiwa amepigwa mara kumi na kutoka sare mara moja.
  Smith, ambaye rekodi yake ni kushinda mapambano 25, akiwa amepigwa mara moja amekuwa akijinoa dhidi ya bondia mkali, Matthew kujiandaa kukabiliana na Matumla ambaye japokuwa ana umri wa miaka 40, lakini ni miongoni mwa mabondia wakali katika uzito wake duniani.
  Ulaya anakumbukwa zaidi kwa vitu alivyofanya mwaka 1999 alipokwenda kutwaa ubingwa wa dunia wa WBU, kwa kumpiga mtu nyumbani kwao, Piacenza, Italia, Paolo Pizzamiglio kwa KO raundi ya pili tu mbele ya mashabiki wake.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MATUMLA AMFUATA SMITH UINGEREZA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top