• HABARI MPYA

  Jumanne, Machi 10, 2009

  MGOSI: AKILI YANGU YOTE ULAYA TU

  Mgosi kulia akiwa na Mwenyekiti wa klabu yake, Simba SC, mzee Hassan Dalali


  MSHAMBULIAJI wa Simba ya Dar es Salaam, Musa Hassan ‘Mgosi’, amesema kwamba hivi sasa akili yake yote ni kucheza soka ya kulipwa Ulaya, baada ya kung’ara kwenye Michuano ya Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN) nchini Ivory Coast.
  Mgosi aliliambia DIMBA mjini Dar es Salaam juzi kwamba uwezo wake wa kusakata soka ni wa kiwango kizuri, kwani kila siku zinavyozidi kusonga mbele anaona mafanikio ya kucheza soka.
  Alisema kilichopo kwake sasa ni kutuliza kichwa ili aweze kutafuta timu ya kuichezea, hasa Ulaya, kwani tayari zaidi ya Watanzania wawili wamemuahidi kumtafutia timu.
  “Awali nilikuwa bado sioni umuhimu wangu katika soka, lakini kadri siku zinavyosonga mbele naona kama ndoto zangu zinaelekea kutimia, maana hata katika fainali ambazo zilifanyika nchini Ivory Coast, kuna Watanzania wanaoishi huko walinifuata na kunisifu huku wakiniahidi kunitafutia timu Ulaya, nafurahia jambo hilo, namwomba Mungu anisaidie,” alisema.
  Aliongeza kwamba yeye kama mchezaji ambaye anaitumikia Simba atahakikisha anaendelea kufanya hivyo hadi hapo mambo yatakapokuwa mazuri, ili atakapopata timu nje ya nchi kufanya majaribio aweze kuondoka kwa baraka kama ilivyokuwa kwa mshambuliaji wa timu hiyo, Danny Mrwanda, anayecheza soka la kulipwa nchini Kuwait.
  “Kwa sasa nipo na timu yangu, nitaendelea kuitumikia kwa moyo mmoja maana najua Simba ndio walezi wangu na kama si wao, si ajabu ningelikuwa sionekani, siwezi kuwadharau viongozi wala kocha wangu ambaye ananisaidia kunipa mawazo ya hapa na pale,” alisema Mgosi.
  Alisema kwa sasa amerudisha makali yake katika Ligi Kuu ya Tanzania Bara ambayo ipo ukingoni kumalizika, ili aweze kuisaidia timu yake iweze kuwa katika nafasi nzuri.
  Mgosi amekuwa mchezaji pekee wa timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars iliyoshiriki CHAN, kuingia kwenye kikosi cha kombaini ya michuano hiyo, tena kama mchezaji wa akiba.
  Katika michuano hiyo iliyomalizika jana kwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kutwaa ubingwa baada ya kuifunga Ghana 2-0, Tanzania ilitolewa Raundi ya Kwanza kwenye kundi lake A, ambalo Zambia na Senegal zilisonga mbele.
  Mshambuliaji wa DRC, Tresor Mputu Mabi, anayewaniwa na Arsenal ya England, ndiye aliyechaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa fainali hizo, wakati mshambuliaji wa Zambia, Given Singuluma, aliibuka mfungaji bora wa CHAN ya kwanza kutokana na kufunga mabao matano.
  Michuano hii ilishirikisha wachezaji wanaocheza Ligi za nyumbani kwao pekee. DRC, mbali na kutwaa ubingwa, pia ilitwaa tuzo ya kucheza soka ya kiungwana uwanjani, Fair Play.
  Kikosi cha CHAN ni; Mamadou Ba (Senegal), Samuel Inkoom (Ghana), Ofusu Appiah (Ghana), Gladys Bokese (DRC), Harrison Afful (Ghana), Jonas Sakuwaha (Zambia), Kazembe Mihayo (DRC), Bongeli Lofo (Drc), Given Singuluma (Zambia), Tresor Mabi Mputu (DRC) Na Moustapha Diallo (Senegal).
  Wachezaji wa akiba ni kipa Samir Abud (Libya), Ovidy Karuru (Zimbabwe), Mussa Mgosi (Tanzania), Ibrahim Ayew (Ghana), Mamadou Baila Traore (Senegal) na Charles Asampong Taylor (Ghana).
  Katika michuano hiyo, Stars iliambulia kutikisa nyavu mara mbili kupitia kwa Mrisho Ngassa, wakati inaibuka na ushindi wa 1-0 dhidi ya wenyeji Ivory Coast na Shadrack Nsajigwa aliyefunga kwa mkwaju wa penalti pale Stars ilipotoka sare ya 1-1 dhidi ya Zambia.

  Taifa Stars ilinikosesha
  kucheza Norway- Uhuru


  KIUNGO wa klabu ya Mtibwa Sugar ya Morogoro, Uhuru Suleiman, amesema kwamba kuumia katika mechi ya kuwania kufuzu Michuano ya Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN) dhidi ya Uganda mjini Mwanza mwaka jana, ndiko kulimkosesha bahati ya kucheza Ulaya.
  Akizungumza na DIMBA juzi mjini Dar es Salaam, Uhuru alisema kwamba akiwa kwenye michuano ya Challenge mwaka juzi, kiwango chake kilimvutia wakala anayetambuliwa na Shirikisho la Soka Ulaya (FIFA), Mehdi Rehmtullah, ambaye aliamua kumpeleka Norway kujaribu bahati yake.
  Uhuru alisema katika safari hiyo aliyokwenda na mshambuliaji wa Burundi, Suleiman Ndikumana, alifuzu majaribio, lakini klabu ya Molde FK ilisema inahitaji muda wa kumpika zaidi kabla ya kuingia naye mkataba.
  “Wakati huo niko Coastal (Union ya Tanga), ikasema nirudi kwanza kuichezea kwenye Ligi ndio baadaye ikiisha niende, nikarudi, niliporudi bahati mbaya ndio nikaingia kwenye CHAN na kuumia, basi hapo ndipo ndoto za Ulaya zilikufa,” alisema.
  Uhuru amesema kwamba kutokana na maumivu yake, hata nafasi yake kwenye timu ya taifa, Taifa Stars imekuwa si nzuri, kwani amekuwa akiitwa na kutemwa kwenye safari.
  “Lakini sasa nipo fiti kabisa, sijakata tamaa, najituma na ninaamini nitapata tena nafasi ya kucheza Ulaya,” alisema mchezaji huyo, aliyekuwamo kwenye kikosi kilichofika Robo fainali ya Challenge mwaka juzi mjini Dar es Salaam.
  Wakati Uhuru bado ‘analikoga’ vumbi la Bara, mwenzake, Ndikumana ameula akiwa anachezea klabu ya Daraja la Pili nchini Ubelgiji, Lierse S.K., aliyojiunga nayo Januari mwaka jana kutoka Molde FK.


  Mwasyika ataka kurejea Oman

  BEKI wa kushoto, Stefano Mwasyika, amesema kwamba baada ya kutua Moro United, sasa anatamani kurejea Oman kucheza soka ya kulipwa, kutokana na maslahi mazuri ya huko.
  Akizungumza na DIMBA juzi mjini Dar es Salaam, Mwasyika ambaye ameitwa tena kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, alisema kwamba alikwama kucheza Oman kutokana na klabu yake ya zamani, Prisons ya Mbeya kumbania.
  Alisema akiwa Moro United, anaamini uongozi wa klabu hiyo hautambana iwapo atapata tena nafasi ya kucheza Oman.
  “Kwanza napenda kutumia nafasi hii kusema kwamba, nimefurahi sana kurejeshwa timu ya taifa, nitatumia nafasi hii kuonyesha uwezo wangu zaidi mbele ya Watanzania,” alisema.
  Mwasyika ni miongoni mwa wachezaji walioitwa kwa ajili ya mchezo wa kirafiki dhidi ya klabu ya Vancouver Whitecaps ya Canada, utakaofanyika Jumamosi wiki hii Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  Wengine ni John Bocco ‘Adebayor’ wa Azam FC, David Naftari wa Simba, George Minja, Shaaban Dihile wa JKT Ruvu, Deogratius Munishi ‘Dida’ wa Simba, Eddy Bushiri wa JKU, Erasto Nyoni (Azam FC), Salum Sued (Mtibwa), Kelvin Yondani, Juma Jabu, Henry Joseph, Jabir Aziz (Simba), Shaaban Nditi (Mtibwa), Nizar Khalfan (Moro United) na Mwinyi Kazimoto (JKT Ruvu), Mussa Hassan ‘Mgosi’ (Simba), Zahoro Pazi na Uhuru Suleiman (Mtibwa).
  Wengine ni wachezaji watano kutoka timu ya vijana chini ya umri wa miaka 20, Razak Khalfan, Khalid Haji, Furaha Yahaya, Haji Ally Nuhu na Ahmed Hassan.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: MGOSI: AKILI YANGU YOTE ULAYA TU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top