• HABARI MPYA

    Friday, March 06, 2009

    NGASSA, NSAJIGWA WAACHA MAJINA CHAN



    NYOTA wa timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Mrisho Ngassa (pichani kulia)na Shadrack Nsajigwa wameingia kwenye historia ya fainali za Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani (Chan) baada ya kila mmoja wao kufunga bao. Katika fainali hizo zilizofanyika katika mji wa Abidjan na Bouake, mshambuliaji wa Zambia, Chipolopolo, Given Singuluma anaongoza kwa upachikaji wa mabao manne. Ngassa alipachika bao lililowazamisha wenyeji wa michuano hiyo, Ivory Coast wakati Nsajigwa alifunga bao kwa njia ya penalti katika mechi dhidi ya Zambia. Aidha, Singuluma alipachika mabao hayo ikiwa ni baada ya kufunga mabao matatu kwenye mechi ya ufunguzi dhidi ya Ivory Coast na bao alilofunga kwenye mechi ya nusu fainali ambayo timu yake ililala kwa mabao 2-1 dhidi ya DRC Congo. Wachezaji wengine ambao wamefunga mabao mawili kila mmoja kutoka Ghana ni Yaw Antwi, Edmund Owusu Ansah na Ibrahim Ayew ambaye ni mtoto wa kwanza wa mchezaji nyota wa zamani, Abeid Pele (Ghana). Wengine ni Alain Kaluyitukadioko na Bongeli Lofo wa DRC Congo na Philip Marufu wa Zimbabwe. Wachezaji ambao kila mmoja alifunga bao moja ni Charles Asampong Taylor (Ghana), Ahmed Osman (Libya), Trésor Mabi Mputu (DRC Congo), Alpha Oumar Sow, Mamadou Baila Traoré (Sénégal), Dennis Banda (Zambia), Ovidy Karuru (Zimbabwe). Aidha, Ghana inaongoza kwa kupachika mabao saba ikifuatiwa na DRC Congo na Zambia ambazo kila moja zimefungwa mabao matano, huku Zimbabwe ikiwa imefunga mabao matatu na Senegal na Tanzania kila moja ikifunga mabao mawili, Libya bao moja, huku safu ya ushambuliaji ya Ivory Coast ikiwa haijaonja nyavu. Hata hivyo, DRC Congo inaongoza kwa kufungwa mabao matano na kufuatiwa na Ivory Coast na Ghana ambazo zimefungwa mabao manne huku Libya, Zambia, Tanzania na Zimbabwe zikifungwa mabao mawili na Senegal ikifungwa bao moja tu. Kwa upande wa nidhamu, Senegal ndio wanaongoza kwa utovu wa nidhamu baada ya kupewa kadi nyekundu moja na za njano tisa na kufuatiwa na Ghana yenye kadi za njano saba na nyekundu moja. Zambia iko nafasi ya tatu ikiwa ina kadi za njano sita na kufuatiwa na DRC Congo na Zimbabwe zenye kadi tano za njano wakati Libya, Tanzania zina kadi nne za njano huku wenyeji Ivory Coast wakiwa na kadi za njano nne na nyekundu moja.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: NGASSA, NSAJIGWA WAACHA MAJINA CHAN Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top