• HABARI MPYA

    Sunday, March 01, 2009

    AMBANI ATIMKIA CHINA


    MPACHIKA mabao tegemeo wa klabu ya Yanga ya Dar es Salaam, Boniphace Ambani (pichani) amesema anaondoka leo mjini Dar es Salaam kwa ndege ya Shirika la Emirates kwenda China kufanya majaribio ya kucheza soka ya kulipwa.
    Akizungumza na DIMBA jana mjini Dar es Salaam, Ambani alisema kwamba safari hiyo inafahamika kwa viongozi wa Yanga ambao wamempa ruhusa na atakuwa huko kwa siku 10.
    “Viongozi wa Yanga wanajua, wameniruhusu,”alisema Ambani ambaye wiki hii ameingia kwenye mgogoro na uongozi wa klabu hiyo juu ya makazi.
    Alisema viongozi wamekosa namna ya kumzuia kwa sababu mkataba wake na klabu hiyo ambao utamalizika mwaka ujao, una kipengele kinachosema akipata timu nyingine asibanwe.
    Alipoulizwa kuhusu kuiacha timu wakati inakabiliwa na mchezo dhidi ya Al Ahly ya Misri, Raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika Machi 13 mjini Cairo, kabla ya timu hizo kurudiana mjini Dar es Salaam wiki mbili baadaye, Ambani alisema: “Kwa njia moja au nyingine, aomba atakayepewa nafasi yangu, afanye vizuri,”alisema.
    Hata hivyo, Mwenyekiti wa Yanga, Imani Madega aliiambia DIMBA kwamba wamemruhusu mchezaji huyo mrefu hadi Machi 6, awe amekwisharejea nchini tayari kuungana na wenzake kwa maandalizi ya mechi dhidi ya Ahly.
    “Kwa kuwa ni majaribio tu, tumeona si vibaya akaenda, kwa sababu kule anakwenda kufanya mazoezi pia, akirudi atakuwa fiti na atakwenda Cairo, itakuwa sawa tu na wale waliopo Ivory Coast,”alisema Madega.
    Hata hivyo, Ambani anaondoka Yanga baada ya kutibuana uongozi wa klabu hiyo, kutokana na sakata la makazi yake.
    “Lilikuwa ni suala dogo ambalo kama viongozi wangekuja mapema, lisingechukua sura ile, lakini tulikuwa tunawapigia simu, hawapokei, lakini kwangu yamekwisha. Naangalia mbele,”alisema.
    Lakini Ambani alisema tangu amerejea nchini Jumanne kutoka kwao, Kenya alipokuwa kwa mapumziko, hajafanya mazoezi hata siku moja kutokana na kutojisikia kufanya hivyo.
    “Siwezi kutia mguu wangu uwanjani kufanya mazoezi wakati nina mkanganyiko wa mawazo, lile suala lilinikera sana, kama wakimbizi bwana,”alisema.
    Ambani alisema bado hajahamia kwenye nyumba aliyopangishiwa yeye na wenzake, Ben Mwalala, Maurice Sunguti na George Owino, kwa sababu haikidhi mahitaji ya kibindamu.
    “Kuna vitu niliwaambia waviweke sawa, kwa mfano feni, Televisheni hakuna kwenye ile nyumba, nitaishije, kitu kama feni, Dar es Salaam ni joto sana, ukiingia tu kwenye ile nyumba hukai, huwezi kulala mle”alisema.
    Kinara huyo wa mabao katika Ligi Kuu ya Bara, alisema kwamba kwa sasa amejipangia mwenyewe hoteli ya Rombo Green View, iliyopo Shekilango Sinza mjini Dar es Salaam.
    Yote kwa yote mchezaji huyo amesema kama atafanikiwa kupata timu China, atakuwa ameiacha Yanga vizuri kwani ni kama tayari amekwishaipa ubingwa kutokana na mabao yake na pia kuivusha hadi Raundi ya Kwanza ya Ligi ya Mabingwa.
    “Nawashukuru wachezaji wenzangu kwa ushirikiano nami, mashabiki kwa kuniunga mkono, makocha pia, mfadhili wa Yanga, (Yussuf Manji), kwa ujumla Tanzania sio pabaya,”alisema.
    Lakini mchezaji huyo amewaasa viongozi nchini kuwaheshimu wachezaji; “Tanzania wanatakiwa waheshimu wachezaji, soka siyo kazi rahisi, wapo wengi wanataka kucheza, lakini hawana vipaji, wewe kiongozi anawaambia wachezaji, we don’t need a star in our team (hatuhitaji nyota kwenye timu yetu).
    Hakuna timu isiyokuwa na star, hata Manchester United, star wao ni Cristiano Ronaldo, lakini mimi sijifanyi star, nilikuwa nazungumzia haki zangu za msingi, makazi,”alisema.
    Ambani ambaye amerejeshwa kwenye timu ya taifa ya nchi yake, Harambee Stars sambamba na wachezaji wenzake wa Yanga, Owino, Mwalala na Barasa alisema atajiunga nayo baada ya majaribio yake China.
    Hadi sasa, Ambani ameifungia Yanga mabao 18 tangu amejiunga nayo, 13 kwenye Ligi, manne kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika na moja kwenye Klabu Bingwa Afrika Mashariki na kati, maarufu kama Kombe la Kagame.
    Wakati huo huo: Kocha wa Yanga, Dusan Kondic kesho anatarajiwa kukutana na Waandishi wa habari kuzungumzia hali halisi ndani ya timu yake, kuelekea kwenye mchezo dhidi ya Ahly.


    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: AMBANI ATIMKIA CHINA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top