• HABARI MPYA

    Saturday, September 07, 2019

    YANGA SC CHUPUCHUPU ‘KULALA NACHO’ KWA PAMBA, YACHOMOA DAKIKA YA MWISHO SARE 1-1

    Na Mwandishi Wetu, MWANZA
    PAMOJA na kucheza pungufu kwa sehemu kubwa ya mchezo, Pamba SC ilikaribia kuwachapa vigogo wa soka Tanzania, Yanga SC baada ya kutoka nao sare ya 1-1 katika mchezo wa kirafiki jioni ya leo Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza.
    Pamba SC inayopambana kurejea Ligi Kuu Tanzania Bara kutoka Daraja la Kwanza, ilifanikiwa kupata bao la kuongoza dakika ya 30 tu, mfungaji mshambuliaji Saad Kipanga aliyemtungua kipa wa tatu, Ramadhani Kabwili akimalizia pasi ya kiungo Nizar Khalfan.
    Pamba SC inayofundishwa na kocha Muhibu Kanu ilipata pigo dakika sita baadaye, kufuatia mchezaji wake, Hamisi Thabit kutolewa kwa kadi nyekundu kwa kosa la kumpiga ngumi kiungo mwenzake, Feisal Salum ‘Fei Toto’ wa Yanga.
    David Molinga amefungua akaunti yake ya mabao Yanga SC leo ikitoa sare ya 1-1 na Pamba SC

    Hata hivyo, Pamba ikafanikiwa kumaliza kipindi cha kwanza bila kuruhusu bao na kuwabana pia mabingwa hao wa kihistoria wa Ligi Kuu ya Tanzania hadi dakika ya mwisho walipowaruhusu kusawazisha.
    Yanga SC ilipata bao la kusawazisha dakika ya 90 na ushei, likifungwa na mshambuliaji David Molinga kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) akimchambua kipa Idrissa Ramadhani baada ya kupokea pasi ya kiungo Deus Kaseke. 
    Na lawama zimuendee Mohammed Mpopo aliyepiga pasi fyongo kwenye eneo lao, mpira ukanaswa na Kaseke aliyempasia Molinga kufunga bao lake la kwanza kabisa tangu asajiliwe Yanga mwezi uliopiuta.
    Kikosi cha Pamba SC kilikuwa; Idrissa Ramadhani, Brian Hizza, Miraj Maka, Mohammed Mpopo, Alex Mwaisaka, Salum Fakhi, Shijja Mkina, Hamisi Thabit, Absalom Chidiebele/Gaudence Mwaikimba dk74, Nizar Khalfan/Rashid Njete dk55 na Saad Kipanga/Amos Matai dk86.
    Yanga SC; Ramadhani Kabwili, Mapinduzi Balama, Ally Mtoni/Muharami Issa ‘Marcelo’ dk59, Ali Ali, Lamine Moro, Feisal Salum, Juma Balinya/Deus Kaseke dk53, Papy Kabamba Tshishimbi, David Molinga, Sadney Urikhob na Mrisho Ngassa/Maybin Kalengo dk73.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: YANGA SC CHUPUCHUPU ‘KULALA NACHO’ KWA PAMBA, YACHOMOA DAKIKA YA MWISHO SARE 1-1 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top