• HABARI MPYA

  Saturday, March 11, 2017

  NIYONZIMA: NILIKWENDA KUSHUGHULIKIA PASIPOTI, NJOONI MUONE KAZI LEO

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  KIUNGO wa Yanga, Haruna Hakizimana Fadhil Niyonzima amesema kwamba alikwenda kushughulikia pasipoti yake mpya baada ya mchezo dhidi ya Simba Februari 25, mwaka huu na sasa amerejea kikamilifu tayari kuendelea kuitumikia timu yake.
  Akizungumza na Bin Zubeiry Sports – Online jana, Niyonzima alisema kwamba alipewa ruhusa na uongozi akashughulikie pasipoti yake na baada ya kufanikisha amerejea kazini.
  Niyonzima hakuonekana tena baada ya Yanga kufungwa 2-1 na Simba Februari 25 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam lakini kwa siku tatu zilizopita ameshiriki mazoezi ya kujiandaa na mchezo wa kwanza wa hatua ya 32 Bora Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Zanaco ya Zambia.
  Haruna Niyonzima amesema kwamba alikwenda kushughulikia pasipoti yake Rwanda

  Mechi hiyo inatarajiwa kufanyika jioni ya leo Uwanja wa Taifa na pamoja na Niyonzima mchezaji mwingine wa Yanga ambaye hajaonekana kwa muda mrefu na aliyekosa hadi mechi dhidi ya Simba, Mzimbabwe Donald Ngoma naye ameshiriki mazoezi.
  Nahodha huyo wa Rwanda, Niyonzima alisema jana kwamba taarifa za mchezaji zinatolewa na timu na fununu na uzushi unaoenezwa kwenye mitandao ya kijamii havina mpango na wala havimuumizi kichwa.
  “Mimi nilikuwa nina ruhusa maalum ya uongozi ya siku tatu kwenda Rwanda kushughulikia pasipoti yangu, nimezitumia vizuri hizo siku tatu na sasa nimerudi,”amesema mchezaji huyo.
  Haruna amewataka mashabiki wa Yanga kujitokeza kwa wingi leo kuisapoti timu ikimenyana na Zanaco Uwanja wa Taifa. “Tumejianda vizuri kwa ajili ya mchezo, mashabiki waje kutusapoti,”amesema.
  Habari njema zaidi kwa kocha Mzambia, George Lwandamina ni kwamba hata kiungo Mzimbabwe, Thabani Kamusoko aliyeumia kwenye mechi dhidi ya Simba naye amefanya mazoezi kuelekea mchezo wa leo.     
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: NIYONZIMA: NILIKWENDA KUSHUGHULIKIA PASIPOTI, NJOONI MUONE KAZI LEO Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top