• HABARI MPYA

    Tuesday, March 07, 2017

    KIINGILIO CHA CHINI AZAM NA MBABANE 3,000 TU

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    KIINGILIO cha chini katika mchezo wa kwanza wa hatua ya 32 Bora Kombe la Shirikisho la Soka Afrikaa kati ya wenyeji, Azam FC na Mbabane Swallows ya Swaziland Jumapili wiki hii kitakuwa Sh. 3,000.
    Mchezo huo utafanyika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam kuanzia Saa 1.15 usiku.
    Ofisa Habari wa Azam FC, Jaffar Idd Maganga amesema leo mjini Dar es Salaam kwamba Sh. 3000 ni kwa mashabiki watakaoketi majukwaa ya mzunguko.
    Maganga amesema eneo la V.I.P B kiingilio kitakuwa ni Sh. 5,000 na V.I.P A itakuwa Sh. 10,000 na mashabiki watanunua tiketi kwa njia ya mtandao kupitia kampuni ya Selcom.
    Nahodha wa Azam FC, John Bocco (kulia) anatarajiwa kuwa fiti kwa mchezo dhidi ya Mbabane
    Maganga amesema wameamua kuuza tiketi hizo mapema, ili kuwarahisishia mashabiki wa soka nchini kupata tiketi hizo kwa haraka na kutosumbuka watakapokuwa wamefunga safari yao kuja kushuhudia mchezo huo.
    “Kama unavyojua uwanja wetu ni mdogo, hivyo kwa kuuza tiketi hizo kwa mfumo huo tutakuwa tumewapunguzia usumbufu mashabiki wa soka kwani idadi kamili ikishatimia ya mashabiki wanaotakiwa basi zoezi la uuzaji tiketi litahitimishwa,” alisema.
    Aidha alitoa wito kwa mashabiki kununua tiketi zao mapema ili kujiwekea uhakika wa kushuhudia uhondo wa mchezo huo kwani hadi sasa watu wengi wamekuwa na shauku kubwa ya kujitokeza uwanjani.
    Katika hatua nyingine, waamuzi watakaochezesha mchezo huo kutoka nchini Benin wanatarajiwa kuwasili nchini Ijumaa hii, ambao ni Mwamuzi wa Kati Adissa Abdul Raphiou Ligali, Mwamuzi Msaidizi Namba Moja, Medegnonwa Romains Agbodjogbe huku Msaidizi Namba Mbili akiwa ni Babadjide Bienvenu Dina. 
    Kikosi cha Azam FC, kinachodhaminiwa na kinywaji safi cha Azam Cola burudani kwa koo lako na Benki bora kabisa nchini ya NMB, kipo kwenye hali nzuri kuelekea mchezo huo kikiwa hakika majeruhi hata mmoja jambo ambalo linatia matumaini makubwa ya timu hiyo kupata matokeo mazuri.
    Jambo pekee ambalo limebakia hivi sasa, ni mashabiki wa soka kwa ujumla wenu nchini hasa jijini Dar es Salaam kujitokeza kwa wingi kuipa sapoti Azam FC kwenye mchezo huo kwani ndio moja ya timu pamoja na Yanga, ambazo zinaiwakilisha Tanzania Bara katika michuano ya Afrika.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KIINGILIO CHA CHINI AZAM NA MBABANE 3,000 TU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top