• HABARI MPYA

  Sunday, April 03, 2016

  TFF SI MALI YA MALINZI, HATUWEZI KUMSUSIA

  WIKI hii, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imekamata gari tano za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kutokana na kushindwa kulipa deni la kodi mbalimbali.
  TRA imekamata gari tano za TFF kutokana na deni la kodi la Sh. Bilioni 1 Milioni 118 ambazo ni malimbikizo tangu mwaka 2010, wakati shirikisho hilo likiwa chini ya Rais Leodegar Tenga.
  Na Rais wa sasa wa TFF, Jamal Malinzi amesema kwamba ana wasiwasi hata Uwanja wa Karume, unaweza kupigwa mnada na TRA kutokana na kwamba gari zilizokamatwa hazifikii thamani ya deni.
  Malinzi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Soka Kagera (KRFA), aliyeingia madarakani Oktoba 28, mwaka 2013 ameonakana kabisa kunyong’onyeshwa na hali hiyo kiasi cha kusema hali ni mbaya. 

  Ofisa wa TRA, Richard Kayombo alikaririwa na vyombo vya Habari akisema kwamba wamekamata gari hizo ili kuwapa shinikizo TFF waweze kulipa madeni hayo yanayotokana na malimbikizo ya kodi mbalimbali kuanzia mwaka 2010 hadi 2015, zikiwemo za VAT na mishahara ya wafanyakazi wake.
  Ikumbukwe Desemba mwaka jana TRA ilizifungia akaunti zote za TFF kutokana na na suala hilo hilo la kodi, wakati huo deni likiwa Sh. Bilioni 1.6, lakini baadaye wakaachiwa baada ya mazungumzo yaliyoihusisha Serikali, kupitia Waziri wa Michezo, Nape Nnauye.
  Hata hivyo, katika hali ya kustaajabisha suala hilo linaibuka upya na safari hii gari za TFF zinakamatwa. 
  Baada ya kukamatwa kwa gari hizo za TFF, Waziri Nape akatoa tamko juzi, kwanza akilisafisha shirikisho hilo kwamba si mdeni halisi wa TRA, bali ni Serikali. 
  Sehemu kubwa ya deni hilo inatokana na kutolipwa kwa kodi za mishahara ya makocha wa timu ya taifa, Taifa Stars na ziara ya timu ya Brazil mwaka 2010, ambayo pia ililetwa na Serikali.
  Nape pia akawaagiza TFF na TRA wakae chini na kufikia makubaliano ya kudumu juu ya deni hilo pamoja na kuwekeana maandishi, ili usumbufu wowote usije ukajitokeza tena.
  Kwa nini haya yanakuja sasa? 
  Tulidhani mazungumzo baina ya viongozi wa TFF na Nape baada ya akaunti za  shirikisho hilo kukamatwa Desemba yalipata suluhisho la kudumu la tatizo hilo.
  Lakini kiumbe hayakuwa na suluhisho wala faida kama miezi mitatu baadaye mambo yanaibuka tena upya.
  Hakuna samahani yoyote katika hilo zaidi ya kusema kuna uzembe ulifanyika ndani ya TFF, ndiyo maana suala hilo limeibuka tena baada ya miezi mitatu.
  Aina hii ya uzembe na upuuzi kwenye mambo mazito kama haya itaendelea siku moja ndoto za Malinzi zitatimia kweli kwa Uwanja wa Karume kupigwa mnada, hususan kipindi hiki cha Serikali isiyo na mzaha ya Rais Dk. John Joseph Pombe Magufuli.
  Inaaminika Malinzi aligombea TFF kwa ukereketwa wake wa soka, dhamira ikiwa ni kuja kuleta mabadiliko katika soka ya Tanzania, lakini kwa mwenendo huu anaweza kugeuka kuwa sumu, iwapo ataendelea kuruhusu uzembe wa aina hii ndani ya shirikisho. 
  Ufike wakati Malinzi sasa aanze kuchukua hatua dhidi ya watendaji wote wazembe ndani ya TFF, ili siku moja shughuli za uendeshaji soka ya nchi hii zipambe moto kwa ujumla.
  Inafahamika TFF inakabiliwa na changamoto nyingi, ikiwemo ukosefu wa fedha za kuendeshea miradi, mazoezi na mipango mbalimbali – maana yake shirikisho linahitaji watu weledi na wabunifu wa hali ya juu ili kujikwamua hapa ilipo.
  TFF kwa sasa haihitaji mashoga wala marafiki wa kiongozi yeyote bali watu wenye uwezo, wabunifu na watendaji wazuri kama inataka kuondoka katika kipindi hiki.
  TFF inahitaji watu wepesi watakaoshughulikia mambo kwa kasi inayotakiwa, ila siku moja Watanzania waje kuifurahia soka yao.
  Katika hili hatuwezi kusema shauri yake Malinzi, kwa sababu TFF si mali yake, bali amepewa dhamana, ambayo walipewa wengine kabla yake na watapewa wengine baada yake, ndiyo maana tunamshauri achukue hatua.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: TFF SI MALI YA MALINZI, HATUWEZI KUMSUSIA Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top