• HABARI MPYA

  Sunday, April 17, 2016

  SIMBA YAKAA KWA TOTO, HALI NI TETE MSIMBAZI

  Na Saada Mohammed, DAR ES SALAAM
  SIMBA inatia huruma. Hiyo ni baada ya kufungwa bao 1-0 na Toto Africans ya Mwanza katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara jioni ya leo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  Kiboko ya Simba leo alikuwa ni kiungo Waziri Junior aliyefunga bao hilo pekee dakika ya 
  20 kwa shuti kali la umbali wa mita 20 lililomshinda kipa Muivory Coast, Vincent Angban.
  Matokeo hayo yanaifanya Simba ishindwe kuwaondoa kileleni mabingwa watetezi, Yanga SC waliorejea juu jana baada ya ushindi wa 1-0 dhidi ya Mtibwa Sugar.
  Shujaa wa Toto leo akiwa amebebwa na mwenzake baada ya filimbi ya mwisho

  Simba inayobaki na pointi zake 57 baada ya kucheza mechi 25, inaendelea kuwa nafasi ya pili, mbele ya Azam FC yenye pointi 55 za meci 24, wakati Yanga wenye pointi 59 za mechi 24 wapo juu. 
  Katika mchezo wa leo, Simba ilicheza pungufu baada ya beki wake wa kulia, Hassan Ramadhani Kessy kutolewa kwa kadi nyekundu dakika ya 47 kwa kumchezea rafu mshambuliaji wa Toto, Edward Christopher.
  Mapema dakika ya 31 kocha wa Simba, Mganda Jackson Mayanja aliondolewa kwenye benchi baada ya kumtolea maneno machafu refa Ahmed Simba wa Kagera.
  Kwa ujumla Simba walizidiwa mchezo leo na hata dalili za kufungwa zilionekana mapema sana. 
  Kikosi cha Simba SC kilikuwa; Vincent Angban, Hassan Kessy, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Novat Lufunga, Hassan Isihaka, Jonas Mkude, Peter Mwalyanzi/Ibrahim Hajib dk38, Awadh Juma, Daniel Lyanga, Hamisi Kiiza na Mussa Mgosi/Emery Nimubona dk50.
  Toto Africans; Mussa Kirungi, Erick Mlilo, Salum Chukwu, Yusuph Mlipili, Hassan Khatib, Carlos Protas, Jama Soud/Salmin Hoza dk56, Abdallah Seseme, Waziri Junior, Edward Christopher/Japhet Vedastus dk72 na Jafari Mohammed/ William Kimanzi dk82.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SIMBA YAKAA KWA TOTO, HALI NI TETE MSIMBAZI Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top