• HABARI MPYA

  Jumamosi, Novemba 07, 2020

  SIMBA SC YALAZIMISHA SARE YA 1-1 NA YANGA DAR, YASAWAZISHA BAO DAKIKA NNE ZA MWISHO

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  MABINGWA watetezi, Simba SC wamenusurika kupoteza mechi mbele ya watani wa jadi, Yanga SC baada ya kulazimisha sare ya 1-1 katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara.
  Kwa sare hiyo, Yanga SC inayofundishwa na Mrundi Cedric Kaze inafikisha pointi 24 na kuendelea kushika nafasi ya pili, ikizidiwa pointi moja na Azam FC, wakati Simba SC inabaki nafasi ya tatu ikifikisha pointi 20 baadaya wote kucheza mechi 10. 
  Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Abdallah Mwinyimkuu aliyesaidiwa na Frank Komba na Mohamed Mkono pembezoni mwa Uwanja na Ramadhani Kayoko na Abubakar Mturo nyuma ya makipa, hadi mapuziko Yanga SC walikuwa mbele kwa bao 1-0.
  Bao hilo lilifungwa na mshambuliaji Mghana, Michael Sarpong kwa mkwaju wa penalti dakika ya 31 baada ya beki Mkenya, Joash Onyango kumuangusha kiungo Tuisila Kisinda kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC). 
  Na ni Yanga SC ndio waliotawala mchezo kipindi cha kwanza na pamoja na kuondoka wanaongoza kwa 1-0, lakini ilipoteza nafasi nyingine za wazi mno kupitia kwa Farid Mussa na Sarpong.


  Kipindi cha pili kibao kikageuka na Simba SC wakauteka mchezo, huku Yanga SC wakicheza kwa kujihami na kushambulia kwa kushitukiza.
  Hata hivyo, safu ya ulinzi ya Yanga SC ikapata pigo baada ya kumpoteza beki wake tegemeo, Mghana Lamine Moro aliyeumia goti na kushindwa kuendelea na mchezo, nafasi yake ikichukuliwa na Said Juma ‘Makapu’ mwanzoni mwa kipindi cha pili.
  Safu ya ulinzi ya Yanga ikapwaya na kuruhusu mashambulizi zaidi ya watani – na haikuwa ajabu Mkenya Onyango alipoisawazishia Simba SC kwa kichwa dakika ya 86 akimalizia kona iliyochongwa na kiungo wa kimataifa wa Msumbiji, Luis Jose Miquissone.
  Kikosi cha Yanga SC kilikuwa; Metacha Mnata, Kibwana Shomari, Yassin Mustafa, Lamine Moro/Said Juma ‘Makapu’ dk50, Bakari Mwamnyeto, Mukoko Tonombe, Tuisila Kisinda, Feisal Salum, Michael Sarpong/Yacouba Sogne dk68, Ditram Nchimbi na Farid Mussa/Zawadi Mauya dk82. 
  Simba SC; Aishi Manula, Shomari Kapombe, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Pascal Wawa, Joash Onyango, Jonas Mkude, Rally Bwalya/Hassan Dilunga dk46, Muzamil Yassin/Ibrahim Ajibu dk85, John Bocco, Clatous Chama na Luis Miquissone.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: SIMBA SC YALAZIMISHA SARE YA 1-1 NA YANGA DAR, YASAWAZISHA BAO DAKIKA NNE ZA MWISHO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top