• HABARI MPYA

  Jumatano, Desemba 11, 2019

  YANGA SC YAKUBALI KUVUNJA MKATABA NA JUMA BALINYA, YAMNG’ANG’ANIA LAMINE MORO

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  KLABU ya Yanga SC imefikia makubaliano ya kuvunja mkataba na mshambulaji wake, Mganda Juma Balinya miezi sita tu tangu ajiunge na timu hiyo kutoka Polisi FC ya kwao. 
  Taarifa ya Yanga SC iliyotolewa leo haikusema sababu za klabu kuachana na mfungaji huyo Bora wa Ligi Kuu ya Uganda msimu uliopita kwa mabao yake 17. 
  “Yanga SC tunamshukuru Balinya kwa huduma yake alipokuwa akiitumikia klabu hii na tunamtakia kila la heri katika maisha yake ya soka huko aendako,”imesema taarifa ya Yanga.

  Ikumbukwe jana Mwenyekiti wa Yanga SC, Dk. Mshindo Msolla alisema kwamba klabu imeridhia ombi la mshambuliaji mwingine, Mnamibia Sadney Urikhob kuvunja mkataba baada ya nusu mwaka pia.
  Lakini Msolla alikanusha madai ya mshambuliaji mwingine, David Molinga ‘Falcao’ kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kuomba kuvunja mkataba.
  Msolla pia alisema klabu haikubaliani na maombi ya beki Mghana, Lamine Moro kutaka kuvunja mkataba kwa sababu bado inamuhitaji na ina mkataba naye.
  Alikiri klabu kushindwa kulipa mishahara ya wachezaji kwa miezi miwili sasa, ingawa alisema hiyo imesababishwa na uongozi wake ulioingia madarakani Me 5, mwaka huu kurithi madeni mengi kutoka kwa watangulizi wao.
  Hata hivyo, Msolla kocha wa zamani wa timu ya taifa ya Tanzania na klabu mbalimbali zikiwemo Milambo FC ya Tabora na Reli Morogoro alisema mchakato wa kulipa mishahara ya miezi miwili umekamilika tangu jana.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: YANGA SC YAKUBALI KUVUNJA MKATABA NA JUMA BALINYA, YAMNG’ANG’ANIA LAMINE MORO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top