• HABARI MPYA

  Jumatatu, Desemba 23, 2019

  AZAM FC YAITOA KWA MATUTA AFRICAN LYON NA KUTINGA HATUA YA 32 BORA MICHUANO YA ASFC

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  MABINGWA watetezi, Azam FC wamekamilisha Hatua ya 64 Bora Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Azam Sports Federation Cup (ASFC) kwa kuitoa African Lyon kwa penalti 4-1 kufuatia sare ya 1-1 ndani ya dakika 90 leo Uwanja wa Uhuru mjini Dar es Salaam leo.
  African Lyon walitangulia kwa bao la Abdallah Muharami dakika ya sita tu, kabla ya Muivory Coast, Richard Ella D’jodi kuisawazishia Azam FC kwa shuti la mpira wa adhabu dakika ya 51.
  Na baada ya dakika ya 90, waliofunga penalti za Azam FC beki Mghana, Yakubu Mohamed, D'jodi, beki Mzimbabwe, Bruce Kangwa na mshambuliaji mzawa, Shaaban Iddi Chilunda, wakati Abdallah Muharami ndiye pekee aliyeifungia African Lyon huku wengine wawili wakikosa.

  Azam FC inaungana na timu nyingine 15 kufuzu Hatua ya 32 Bora ya ASFC, ambazo ni washindi wa pili wa msimu uliopita, Lipuli FC, mabingwa wengine wa zamani wa Kombe hilo, Yanga, Simba SC na Mtibwa Sugar.
  Timu nyingine zilizotinga 32 Bora ni Kagera Sugar, Polisi Tanzania, Ruvu Shooting, Alliance FC, Mbeya City, Ndanda FC, Namungo FC, JKT Tanzania, Mwadui FC, Tanzania Prisons, KMC na Biashara United.
  Nyingine ni African Sports, Stand United, Maji Maji, Ihefu FC, Mighty Elephant, Gwambina FC, Mawenzi Market, Gipco FC, Pan Africans, Panama FC, Jeshi Warriors, Sahare All Stars, Friends Rangers, Kitayosa United na Tukuyu Stars.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: AZAM FC YAITOA KWA MATUTA AFRICAN LYON NA KUTINGA HATUA YA 32 BORA MICHUANO YA ASFC Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top