• HABARI MPYA

  Jumatano, Desemba 25, 2019

  SIMBA SC YAENDELEZA ‘UMWAMBA’ LIGI KUU YA TANZANIA BARA, YAITANDIKA LIPULI FC 4-0 UHURU

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  MABINGWA watetezi, Simba SC wameendeleza ‘dozi’ baada ya leo kuwachapa Lipuli FC ya Iringa 4-0 katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara Uwanja wa Uhuru mjini Dar es Salaam.
  Ushindi huo wa pili mfululizo chini ya kocha mpya, Mbelgiji Sven Ludwig Vandenbroeck unaifanya Simba SC ifikishe pointi 28 katika mchezo wa 11 na kuendelea kuongoza Ligi Kuu kwa pointi nne zaidi ya Kagera Sugar inayofuatia ambayo pia imecheza mechi mbili zaidi.
  Ikitoka kuichapa AFC ya Arusha 6-0 katika mchezo wa kwanza chini ya Vandenbroeck, Simba SC leo iliendelea kucheza soka safi ya pasi za haraka na kasi ya kushambulia kiasi cha kuwazidi kabisa wapinzani.

  Kiungo wa kimatafa wa Kenya, Francis Kahata Nyambura aliye katika msimu wa kwanza tangu awasili kutoka Gor Mahia ya kwao ndiye aliyefungua shangwe za za mabao leo akifunga dakika ya 11 baada ya pasi nzuri ya beki mzawa, Shomari Salum Kapombe.  
  Mkongwe mwenye umr wa miaka 33, Meddie Kagere Mlewa Msasa akaifungia Simba SC bao la pili dakika ya 49 akimalizia pasi ya kiungo Mzambia, Clatous Chota Chama.
  Ndipo ikawadia zamu ya kiungo wa kimataifa wa Tanzania, Hassan Saleh Dilunga kufunga mabao mawili mfululizo kukamilisha ushindi mnono wa Wekundu wa Msimbazi.
  Dilunga, mchezaji wa zamani Ruvu Shooting, Yanga SC na Mtibwa Sugar alifunga bao la tatu kwa penalti dakika ya 57 baada ya beki wa Lipuli FC, Novaty Lufunga kuunawa mpira kwenye boksi na la nne akafunga akimalizia pasi ya kiungo wa kimataifa wa Sudan, Sharaf Eldin Shiboub. 
  Kikosi cha Simba SC kilikuwa; Beno Kakolanya, Shomari Kapombe, Gardiel Michael, Tairone Santos, Paschal Wawa/Kennedy Juma dk73, Jonas Mkude/Muzamil Yassin dk63, Hassan Dilunga, Sharaf Shiboub, Meddie Kagere, Clatous Chama na Francis Kahata/Deo Kanda dk63.
  Lipuli FC; Agathon Anthony, David Kameta, Emannuel Kichiba/Joshua Ibrahim dk86, David Mwasa, Novaty Lufunga, Fredy Tangalo, Mwinyi Ahmed/Shaban Ada dk65, Steven Mgayu, Paul Nonga, Daruwesh Saliboko/Issah Ngoah dk84 na Keneth Masumbuko.   
  Mchezo mwingine wa Ligi Kuu leo, Polisi Tanzania imeibuka na ushindi wa 2-1 dhidi ya KMC Uwanja wa Ushirika mjini Moshi, mabao ya timu ya Kilimanjaro yakifungwa na Marcel Kaheza dakika ya 21 kwa penalti na Erick Msagati dakika ya 78, wakati la timu ya Kinondoni limefungwa na Abdul Hilary kwa penalti pai dakika ya 81. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: SIMBA SC YAENDELEZA ‘UMWAMBA’ LIGI KUU YA TANZANIA BARA, YAITANDIKA LIPULI FC 4-0 UHURU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top