• HABARI MPYA

  Jumanne, Desemba 31, 2019

  SIMBA SC ‘YAWATISHA WATANI’, YAWACHAPA NDANDA FC 2-0 WAFUNGAJI KAHATA NA DEO KANDA

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  MABINGWA watetezi, Simba SC wameendeleza ubabe katika Ligi Kuu ya Tanzania Bara baada ya ushindi wa 2-0 dhidi ya Ndanda FC jioni ya leo Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
  Kwa ushindi huo, Simba SC iliyo chini ya kocha Mbelgiji, Sven Ludwig Vandenbroeck anayesaidiwa na mchezaji wa zamani wa klabu hiyo, inafikisha pointi 34 katika mchezo wa 13, ikiendelea kuongoza Ligi Kuu kwa pointi 10 zaidi ya watani wao wa jadi, Yanga SC ambao hata hivyo wana mechi mbili mkononi.
  Katika mchezo wa leo ambao Simba SC ilimuacha benchi kwa muda wote kinara wake wa mabao, Mnyarwanda, Meddie Kagere – ilipata bao moja kila kipindi na yote yakifungwa na wachezaji wake wa kigeni.


  Aliyefungua shangwe za mabao leo Uwanja wa Taifa alikuwa ni kiungo wa kimataifa wa Kenya, Francis Kahata Nyambura aliyemtungua kipa wa zamani wa Simba SC, Ally Mustafa ‘Barthez’ kwa kufunga bao la kwanza kwa shuti la mpira wa adhabu dakika ya 13.
  Kiungo anayecheza kwa mkopo kutoka klabu ya TP Mazembe ya kwao, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Deo Kanda akahitimisha shangwe za mabao kwa kumtungua Barthez aliyewahi kudakia na Yanga pia dakika ya 85 akimalizia pasi ya beki wa kushoto Gardiel Michael Kamagi.
  Simba SC ingeweza kuondoka na ushindi mnono zaidi leo kama ingetumia vyema nafasi zake nyingine mbili nzuri ilizotengeneza.
  Mechi nyingine ya Ligi Kuu ya leo, Mwadui FC imelazimishwa sare ya 1-1 na KMC Uwanja wa Kambarage, Shinyanga. Abdul Hillary alianza kuifungia KMC dakika ya 25, kabla ya Enock Mkanga kuisawazishia Mwadui dakika ya 71.  
  Kikosi cha Simba SC kilikuwa; Aishi Manula, Haruna Shamte, Gardiel Michael, Erasto Nyoni, Kennedy Juma, Jonas Mkude/Muzamil Yassin dk65, Ibrahim Ajibu/Clatous Chama dk78, Said Hamisi Ndemla, John Bocco, Sharaf Shiboub na Francis Kahata/Deo Kanda dk56.
  Ndanda FC; Ally Mustafa ‘Barthez’, Shaffi Naimu/Azizi Sibo dk90, Said Mbatty, Samuel Mauru, Paul Maona, Hemed Khoja, Godfrey Malibiche, Taro Joseph, Nassor Saleh/Omary Ramadhan dk74, Kiggi Makassy na Omar Hassan.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: SIMBA SC ‘YAWATISHA WATANI’, YAWACHAPA NDANDA FC 2-0 WAFUNGAJI KAHATA NA DEO KANDA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top