• HABARI MPYA

  Jumatano, Desemba 18, 2019

  AZAM FC YAWAONGEZEA MIKATABA KIPAGWILE NA MWADINI HADI, YAMTUPIA VITRAGO NDIKUMANA

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  WINGA machachari, Idd Kipagwile ameongeza mkataba mpya wa miaka miwili kuendelea kuitumikia klabu ya Azam FC, mabingwa wa Kombe la Shiriksho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Azam Sports Federation Cup (ASFC).
  Kipagwile anayesifika kwa mashuti, kuchachafya mabeki na kasi yake uwanjani, atabakia kutoa huduma yake ndani ya viunga vya Azam Complex hadi mwaka 2022.
  Huyo anakuwa mchezaji wa pili kuongeza mkataba ndani ya kipindi hiki cha usajili wa dirisha dogo, baada ya kipa Mwadini Ally aliyeongeza mkataba wa mwaka mmoja.
  Mkataba wake pia amesaini leo Jumanne mbele ya Ofisa Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Abdulkarim Amin 'Popat', utamfanya Mwadini kusalia kwa wababe hao kutoka Azam Complex hadi Julai 2021.
  Mwadini amekuwa sehemu ya mafanikio ya kikosi cha Azam FC tokea ajiunge nayo mwaka 2011 akitokea Mafunzo ya Zanzibar, ambapo kikosini kwa sasa amekuwa akisaidiana na makipa wenzake, Razack Abalora na Benedict Haule.
  Katika hatua nyingine, Azam FC imethibitisha kuachana na aliyekuwa mshambuliaji wake, Suleiman Ndikumana, baada ya kufikia makubaliano ya pande zote mbili.
  Ndikumana aliyejiunga na Azam FC kwenye dirisha lililopita la usajili mwezi Juni mwaka huu, ameamua kuondoka ili akasake changamoto nyingine na kuendeleza kipaji chake, baada ya kushindwa kupata nafasi ipasavyo ndani ya kikosi hicho. “Tunapenda kumtakia kila la kheri katika maisha yake mapya ya soka popote aendako,” imesema taarifa ya Azam FC.
  Wakati huo huo: Azam FC imemtambulisha, Tunga Ally, kuwa Meneja Mkuu wake wa Masoko katika harakati za kuongeza ufanisi kwenye utendaji kazi ndani ya klabu hiyo.
  Utambulisho wake huo, umefanywa leo na Ofisa Mtendaji Mkuu, Abdulkarim Amin 'Popat', aliyekuwa sambamba na Makamu Mwenyekiti wa timu hiyo, Omary Kuwe.
  Ally atakuwa na majukumu ya moja kwa moja ya kuandaa mipango ya uuzwaji wa vifaa vya Azam FC kwa mashabiki wa timu hiyo na Watanzania kiujumla.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: AZAM FC YAWAONGEZEA MIKATABA KIPAGWILE NA MWADINI HADI, YAMTUPIA VITRAGO NDIKUMANA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top