• HABARI MPYA

  Jumapili, Desemba 22, 2019

  SIMBA SC YAFANYA ‘MAUWAJI’ AZAM SPORTS FEDERATION CUP, YAITANDIKA AFC ARUSHA 6-0 DAR

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  SIMBA SC imefanikiwa kuvuka Hatua ya 32 Bora ya Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Azam Sports Federaton Cup (ASFC) kwa mara ya kwanza ndani ya miaka mitatu baada ya ushindi wa 6-0 dhidi ya AFC ya Arusha leo Uwanja wa Uhuru mjini Dar es Salaam.
  Mwaka juzi Simba SC ilitolewa kwa penalti na Green Warriors ya Mwenge, Dar es Salaam na mwaka jana ikatolewa na Mashujaa ya Kigoma, zote timu za Jeshi katika hatua kama hii, lakini leo wamevunja mwiko.   
  Kiungo Mzambia, Clatous Chama alifungua shangwe za mabao dakika ya 18 akimalizia mpira uliotemwa na kipa Athumani Nyamaka baada ya shuti la mshambuliaji wa kimatafa wa Rwanda, Meddie Kagere.


  Mbrazil, Gerson Fraga ‘Viera’ akafunga bao la pili dakika ya 23 akimalizia pasi ya mzawa, Ibrahim Ajibu baada ya kona ya kiungo mwenzao, Mkenya Francis Kahata.
  Kiungo kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Deogratius Kanda akafunga bao la tatu dakika ya 27 akimalizia pasi ya fundi wa mpira, Ajibu ambaye alifunga bao la nne dakika ya 33 akimalizia pasi ya Chama.
  Kinara wa mabao wa Simba SC, Kagere akafunga bao la tano dakika ya 56 akimalizia mpira uliotemwa na kipa Nyamaka baada ya shuti la mchezaji mwenzake wa zamani wa Gor Mahia ya Kenya, Kahata ambaye alifunga bao la sita dakika ya 66 akimalizia krosi ya Kanda.
  Kikosi cha Simba SC kilikuwa; Beno Kakolanya, Shomari Kapombe/Kennedy Wilson Juma dk57, Haruna Shamte, Tairone Santos, Pascal Wawa, Gerson Fraga, Deo Kanda, Clatous Chama/Sharaf Shiboub dk58, Meddie Kagere/Wilker Da Silva dk57, Ibrahim Ajibu na Francis Kahata.
  AFC; Athumani Nyamaka, Said Shilingi, Shaaban Mtangi, Salum Mtambo, Rodney Chitopela, James Shangala, John Mbilinyi, Jonathan Masimba/Andrew Pastima dk47, Ajib Mohamed, Mathayo Wilson/Dickson Kalinga dk61 na Gasper Mwaipasi.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: SIMBA SC YAFANYA ‘MAUWAJI’ AZAM SPORTS FEDERATION CUP, YAITANDIKA AFC ARUSHA 6-0 DAR Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top