• HABARI MPYA

  Jumatatu, Septemba 09, 2019

  SAMATTA: JAPO NJIA YA USHINDI ILIKUWA NGUMU, LAKINI TAIFA STARS TUMEPATA TULICHOKITAKA

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  NAHODHA wa Tanzania, Mbwana Ally Samatta amerejea Ubelgiji kuitumikia klabu yake, KRC Genk huku akiwashukuru wananchi kwa sapoti yao kwa timu ya taifa hadi ikafanikiwa kuitoa Burundi katika kinyanganyiro cha tiekti ya Fainali za Kombe la Dunia 2022 nchini Qatar.
  Samatta aliitanguliza Taifa Stars kwa bao lake la dakika ya 30 akimalizia kona ya beki wa kulia, Hassan Ramadhani Kessy anayechezea Nkana FC ya Zambia, kabla ya Abdulrazak Fiston kuisawazishia Burundi dakika ya 45 akimalizia kazi nzuri ya mshambuliaji chipukizi, Amissi Mohammed.
  Mchezo huo ukamalizika kwa sare ya 1-1 na kufanya sare ya jumla ya 2-2 kufuatia sare nyingine ya 1-1 mjini Bujumbura Jumatano iliyopita na Tanzania ikaenda kushinda kwapenalti 3-0 jana Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
  Nahodha wa Tanzania, Mbwana Ally Samatta akipasua katikati ya wachezaji wa Burundi jana

  Beki mkongwe anayeweza kucheza kama kiungo pia, Erasto Edward Nyoni alianzisha biashara nzuri kwa Taifa Stars baada ya kufunga penalti ya kwanza na wenzake, kiungo Himid Mao Mkami ‘Ninja’ na beki Gardiel Michael Mbaga wakafunga pia.
  Kaseja aliwakata maini Warundi baada ya kuokoa penalti ya kwanza ya Int’hamba Murugamba iliyopigwa na mtokea benchi, Gael Duhayindavyi aliyetokea benchi kuchukua nafasi ya Kanakimana Bienvenu Kanakimana dakika ya 67 na haikuwa ajabu Saido Berahino na Bigirmana Gael wakapiga nje mfululizo. 
  Na baada ya mchezo huo, Samatta amesema; “Japo njia ya ushindi ilikuwa ngumu, lakini mwisho tulipata tulichokitaka kama Nahodha nikiwakilisha wachezaji wenzangu pamoja na benchi la ufundi tutakuwa wachoyo wa fadhila tusipowashukuru nyote mliojitokeza katika michezo hii miwili dhidi ya Burundi,”.
  “Sapoti yenu ilitusukuma pale ambapo kulilega na matokeo haya ya kufuzu hatua ya makundi tunayaelekeza kwenu Watanzania wote mnaoisapoti timu ya taifa kwa moyo wa dhati, hata wale ambao hawakupata bahati ya kufika uwanjani, na popote walipokuwa waliomba ushindi kwa moyo mmoja na pia kwa wote ambao kwa njia moja ama nyingine walitumia njia yoyote kuhamasisha wengine kuisapoti timu yao. Asante sana. Viva Taifa Stars,” aliongeza.
  Taifa Stars inaungana na washindi wengine 13 wa hatua ya mchujo kuungana na timu nyingine 26 za viwango vya juu barani, wakiwemo majirani Kenya na Uganda kuingia kwenye makundi 10 kuanza rasmi kuwania tiketi ya Qatar 2022.
  Washindi 10 wa kwanza wa makundi yote watamenyana baina yao katika hatua ya tatu na ya mwisho mchujo wa mbio hizo za Qatar na timu tano zitakazoshinda ndizo zitaiwakilisha Afrika katika Kombe la Dunia lijalo.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: SAMATTA: JAPO NJIA YA USHINDI ILIKUWA NGUMU, LAKINI TAIFA STARS TUMEPATA TULICHOKITAKA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top