• HABARI MPYA

  Jumanne, Februari 27, 2018

  BODI YA LIGI YAIPA AHUENI YANGA MAANDALIZI LIGI YA MABINGWA, YAAHIRISHA MECHI NA MTIBWA

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  MCHEZO wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kati ya wenyeji Mtibwa Sugar na Yanga SC ya Dar es Salaam uliopangwa kufanyika Machi 3, mwaka huu Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro umeahirishwa. 
  Sababu za kuuahirisha mchezo huo namba 170 ni kuipa Yanga nafasi nzuri ya maandalizi ya mchezo wake wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Township Rollers ya Botswana Machi 6 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  Busara za Bodi chini ya Mwenyekiti wake, Clement Sanga ambaye pia ni Kaimu Mwenyekiti wa Yanga SC zimeielekeza kuusogeza mbele mchezo wa Ligi Kuu ili kuwapa wawakilishi hao wa Tanzania kwenye Ligi ya Mabingwa fursa nzuri ya maandalizi. 
  Baada ya kukata tiketi ya Robo Fainali ya michuano ya Azam Sports Federation Cup (ASFC) kufuatia ushindi wa 2-1 dhidi ya wenyeji, Maji Maji Uwanja wa Maji Maji mjini Songea Jumapili, Yanga iliondoka mjini humo mapema Jumatatu kwa basi lake kwenda Mtwara tayari kwa mchezo mwingine wa Ligi Kuu dhidi ya wenyeji, Ndanda FC Jumatano Uwanja wa Nangwanda Sijaona.
  Mabao ya Yanga Jumapili yalifungwa na kiungo Pius Charles Buswita kwa kichwa dakika ya 40 akimalizia krosi ya beki Mwinyi Hajji Mngwali kutoka upande wa kushoto baada ya kuanzishiwa kona fupi na kiungo mwenzake, waliyekuwa wakicheza naye pale mbele, Ibrahim Ajib na winga Emmanuel Martin dakika ya 57 akimalizia kwa kichwa krosi ya beki wa kulia, Hassan Kessy aliyemlamba chenga Mpoki Mwakinyuki.
  Bao pekee la Maji Maji lilifungwa na kiungo Jaffar Mohammed kwa kichwa dakika ya 61, akimalizia mpira wa adhabu uliopigwa na beki Aziz Sibo kufuatia Nahodha, Kevin Yondan kumchezea rafu Marcel Boniventura.
  Yanga ilikata tiketi ya kwenda Raundi ya Kwanza ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika Jumatano iliyopita licha ya sare ya 1-1 na wenyeji, Saint Louis Suns United katika mchezo wa marudiano wa Raundi ya Awali Uwanja wa Linite.
  Mabingwa hao wa Tanzania wamesonga mbele kwa ushindi wa jumla wa 2-1 baada ya Februari 10 kushinda 1-0 pia Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, bao pekee la kiungo Juma Mahadhi aliyekosekana uwanjani kwenye mechi ya marudiano kwa sababu ya homa.
  Kwa kuitoa St Louis, Yanga itakutana na Township Rollers ya Botswana katika Raundi ya Kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika, ambayo nayo iliitoa El Merreikh ya Sudan, mechi ya kwanza ikichezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam Machi 6 kabla ya kwenda Gaborone kwa mchezo wa marudiano, Machi 17.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: BODI YA LIGI YAIPA AHUENI YANGA MAANDALIZI LIGI YA MABINGWA, YAAHIRISHA MECHI NA MTIBWA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top