• HABARI MPYA

  Jumapili, Februari 25, 2018

  WYDAD WABEBA SUPER CUP BAADA YA KUIPIGA MAZEMBE 1-0

  BAO la mpira wa adhabu la Amin Tighazoui dakika ya 83 limeipa ushindi wa 1-0 Wydad Casablanca dhidi ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kwenye mchezo wa kuwania taji la Super Cup ya CAF usiku wa jana Uwanja wa Mohammed V mjini Casablanca, Morocco.
  Katika mchezo huo ambao teknolojia ya msaada wa picha za video kwa marefa (VAR) ilitumika kwa mara ya kwanza barani Afrika, Wydad imekata kiu yake ya muda mrefu ya kutwaa taji hilo.
  Mzaliwa huyo wa Ufaransa, Tighazoui, ambaye hakuwemo kwenye kikosi cha Wydad kilichotwaa taji la Ligi ya Mabingwa Novemba mwaka jana, alipiga vizuri kiutalaamu mpira wake wa adhabu uliopenya ukuta wa Mazembe na kwenda kumpita kipa Sylvain Gbohouo.
  Kipa Muivory Coast wa Mazembe, Gbohouo aliokoa mkwaju wa penalti wa Walid el Karti dakika ya 55.
  Ushindi wa Wydad Casablanca ni muendelezo wa mafanikio ya Morocco katika soka yaliyoanza Novemba mwaka jana walipoifunga Al Ahly ya Misri na kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa Afrika kwa mara ya pili katika historia yao.
  Timu ya taifa ya Morocco nayo, Simba wa Atlasi ikafuzu Fainali za Kombe la Dunia chini ya kocha Mfaransa, Herve Renard mwezi huo huo na timu ya wachezaji wa nyumbani imetwaa taji la CHAN siku 20 zilizopita.
  Kwa kutwaa taji la Super Cup kwa mara ya kwanza, Wydad inamfanya kocha Mtunisia, Faouzi Benzarti awe kocha wa pili kwa mafanikio makubwa barani kutona ana kutwaa mataji matano ya CAF.
  Ametwaa mataji mawili akiwa na Esperance na mawili mengine akiwa na klabu nyingine ya Tunisia, Etoile Sahel, kabla ya kuchukuliwa na Wydad mwaka huu baada ya kufukuzwa kwa Hussein Amoutta kutokana na matokeo mabaya kwenye Ligi ya nyumbani.
  Mreno Manuel Jose anashikilia rekodi ya kutwaa mataji mengi ya ngazi ya klabu barani, akiiwezesha Al Ahly kutwaa mataji manne ya Ligi ya Mabingwa na manne ya Super Cup. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: WYDAD WABEBA SUPER CUP BAADA YA KUIPIGA MAZEMBE 1-0 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top