• HABARI MPYA

  Jumapili, Februari 25, 2018

  MTIBWA SUGAR WAIPIGA BUSERESERE 3-0 NYAMAGANA NA KUTINGA NANE BORA ASFC

  Na Mwandishi Wetu, MWANZA
  TIMU ya Mtibwa Sugar imefanikiwa kwenda Robo Fainali ya michuano ya Azam Sports Federation Cup (ASFC) baada ya ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya wenyeji, Buseresere FC Uwanja wa Nyamagana mjini Mwanza mchana wa leo.
  Baada ya dakika 45 ngumu za kipindi cha kwanza, Mtibwa Sugar walianza kuimiminia mabao mfululizo Buseresere FC kipindi cha pili.
  Kiungo wa zamani wa Yanga, Hassan Dilunga alifunga bao la kwanza dakika ya 52 kwa penalti baada ya yeye mwenyewe kuangushwa kwenye boksi, kabla ya winga wa zamani wa Simba, Haroun Athuman Chanongo aliyembadili mshambuliaji Stahmil Mbonde kipindi cha pil kufunga la pili dakika ya 82 akimalizia krosi ya Salum Kihimbwa.
  Kiungo Ally Makalani akakamilisha shangwe za mabao za Mtibwa Sugar ya kocha Zuberi Katwila kwa kufunga bao la tatu dakika ya 90 kwa shuti la umbali wa mita 19 kufuatia pasi ya Haroun Chanongo, kabla ya Buseresere kupata pigo dakika ya tatu ya muda wa nyongeza baada ya kutimia dakika 90 za kawaida kwa mshambuliaji wake, John Evarest ‘Utaka’ kutolewa kwa kadi nyekundu kufuatia kuonyeshwa kadi ya pili ya njano.
  Mtibwa Sugar inakuwa timu ya nne kwenda Robo Fainali ya michuano hiyo, baada ya Azam FC iliyoitoa KMC ya Kinondoni kwa kuichapa mabao 3-1 jana, Singida United iliyoitoa Polisi Tanzania jana pia kwa kuifunga mabao 2-0 Uwanja wa Namfua, Singida na Njombe Mji FC iliyowatoa Mbao FC Jumatano kwa penalti 6-5 kufuatia sare ya 1-1.
  Hatua ya 16 Bora ya ASFC inaendelea jioni hii, Maji Maji wakuikaribisha Yanga Uwanja wa Maji Maji mjini Songea kuanzia Saa 10:00 na Saa 1:00 usiku, JKT Tanzania watamenyana na Ndanda FC Uwanja wa Azam Complex Chamazi, Dar es Salaam.
  Mechi za 16 Bora ya ASFC zitakamilishwa kesho kwa Kiluvya United kuwakaribisha Tanzania Prisons Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani kuanzia Saa 8:00 mchana na Stand United watakuwa wenyeji wa Dodoma FC Uwanja wa Kambarage, Shinyanga Saa 10:00 jioni.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: MTIBWA SUGAR WAIPIGA BUSERESERE 3-0 NYAMAGANA NA KUTINGA NANE BORA ASFC Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top