• HABARI MPYA

  Jumapili, Februari 25, 2018

  YANGA SC WAICHAPA MAJI MAJI 2-1 SONGEA NA KUTINGA NANE BORA AZAM SPORTS FEDERATION

  Na Mwandishi Wetu, SONGEA
  YANGA SC wamekata tiketi ya Robo Fainali ya michuano ya Azam Sports Federation Cup (ASFC) baada ya ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya wenyeji, Maji Maji katika mchezo wa mkondo mmoja uliofanyika Uwanja wa Maji Maji mjini Songea jioni ya leo.
  Katika mchezo huo uliochezeshwa na marefa  Benedicto Magai aliyesaidiwa na Mashaka Mwandemba na Michael Mkongwa, hadi mapumziko Yanga SC walikuwa mbele kwa bao 1-0.
  Bao hilo lilifungwa na kiungo mshambuliaji, Pius Charles Buswita kwa kichwa dakika ya 40 akimalizia krosi ya beki Mwinyi Hajji Mngwali kutoka upande wa kushoto baada ya kuanzishiwa kona fupi na kiungo mwenzake, waliyekuwa wakicheza naye pale mbele, Ibrahim Ajib.
  Emmanuel Martin (kulia) amefunga bao la pili leo Yanga ikishinda 2-1 dhidi ya Maji Maji mjini Songea

  Pamoja na kumaliza kipindi cha kwanza ikiwa inaongoza kwa bao 1-0, lakini ni Maji Maji waliotawala zaidi mchezo, wakakosa tu umakini wa kumalizia mipango yao.
  Na mchezo wa Yanga wa kuwategeshea mitego ya kuotea wachezaji wa Maji Maji kwa kiasi kikubwa ilifanikiwa kipindi cha kwanza.
  Kipindi cha pili, Yanga walirejea na mchezo wa umakini wakishambulia na kujilinda kwa tahadhari ya hali ya juu dhidi ya wenyeji, waliokuwa wakicheza kwenye Uwanja mbovu waliouzoea.
  Haikuwa ajabu Yanga walipofanikiwa kupata bao la pili lililofungwa na winga Emmanuel Martin dakika ya 57 akimalizia kwa kichwa krosi ya beki wa kulia, Hassan Kessy aliyemlamba chenga Mpoki Mwakinyuki.
  Yanga SC wakaonekana kuridhika baada ya bao hilo na Maji Maji wakatumia fursa hiyo kutafuta bao walilolafanikiwa kulipata dakika ya 61 kupitia kwa kiungo Jaffar Mohammed aliyefunga kwa kichwa akimalizia mpira wa adhabu uliopigwa na beki Aziz Sibo kufuatia Nahodha, Kevin Yondan kumchezea rafu Marcel Boniventura.
  Yanga SC inakuwa timu ya tano kuingia Nane Bora ya Azam Sports Federation baada ya Mtibwa Sugar iliyoiengua Buseresere FC kwa kuichapa 3-0 kwenye mchezo uliotangulia mchana wa leo, Azam FC iliyoitoa KMC ya Kinondoni kwa kuichapa mabao 3-1, Singida United iliyoitoa Polisi Tanzania kwa kuifunga 2-0 jana Uwanja wa Namfua, Singida na Njombe Mji FC iliyowatoa Mbao FC Jumatano kwa penalti 6-5 kufuatia sare ya 1-1.
  Hatua ya 16 Bora ya ASFC inaendelea Saa 1:00 usiku leo kwa JKT Tanzania kuwakaribisha Ndanda FC Uwanja wa Azam Complex Chamazi, Dar es Salaam.
  Mechi za 16 Bora ya ASFC zitakamilishwa kesho kwa Kiluvya United kuwakaribisha Tanzania Prisons Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani kuanzia Saa 8:00 mchana na Stand United watakuwa wenyeji wa Dodoma FC Uwanja wa Kambarage, Shinyanga Saa 10:00 jioni.
  Kikosi cha Maji Maji FC leo kilikuwa; Saleh Malande, Aziz Sibo, Mpoki Mwakinyuki, Juma Salamba, Idrisa Mohammed, Hassan Hamisi, Lucas Kikoti, Yakubu Kibiga, Marcel Boniventura, Peter Mapunda na Jafar Mohammed/Paul Lyungu dk85.
  Yanga SC; Youthe Rostand, Hassan Kessy, Mwinyi Mngwali, Kelvin Yondan, Said Juma ‘Makapu’, Raphael Daudi/Yussuf Mhilu dk71, Pato Ngonyani, Papy Kabamba Tshishimbi, Pius Buswita, Ibrahim Ajib na Emmanuel Martin/Geofffrey Mwashiuya dk88.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: YANGA SC WAICHAPA MAJI MAJI 2-1 SONGEA NA KUTINGA NANE BORA AZAM SPORTS FEDERATION Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top