• HABARI MPYA

  Alhamisi, Februari 22, 2018

  NAHODHA YANGA, NADIR HAROUB 'CANNAVARO' AFIWA NA MWANAWE MUHIMBILI

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  NAHODHA wa Yanga SC, Nadir Haroub Ali ‘Cannavaro’ amefiwa na mtoto wake, Anuar aliyekuwa anapatiwa matibabu katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Dar es Salaam.
  Taarifa fupi ya Yanga SC kwa vyombo vya Habari leo imesema kwamba, taarifa zaidi zitafuatia baadaye kutoka kwenye familia. 
  Msiba huu mzito unamkuta Cannavaro aliyeingia mwaka 2006 siku moja baada ya kuisaidia klabu yake kwenda Raundi ya Kwanza ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika licha ya sare ya 1-1 na wenyeji, Saint Louis Suns United jana jioni katika mchezo wa marudiano wa Raundi ya Awali Uwanja wa Linite mjini Victoria, Shelisheli.
  Pole Nahodha, Nadir Haroub Ali ‘Cannavaro’ kwa kufiwa na mwanao 

  Mabingwa wa Tanzania wamesonga mbele kwa ushindi wa jumla wa 2-1 baada ya Februari 10 kushinda 1-0 pia Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, bao pekee la kiungo Juma Mahadhi aliyekosekana uwanjani leo kwa sababu ya homa.
  Katika mchezo wa leo uliochezeshwa na marefa Madagascar, Andofetra Avombitana Rakotojaona aliyesaidiwa na Lionel Hasinjarasoa Andrianantenaina na Pierre Jean Eric Andrivoavonjy, hadi maopumziko Yanga walikuwa mbele kwa bao 1-0.
  Bao hilo lilifungwa na kiungo mshambuliaji mjuzi wa kuuchezea mpira, Ibrahim Ajib Migomba dakika ya 45 akimalizia krosi nzuri ya beki wa kulia, Hassan Ramadhan Hamisi ‘Kessy’.
  Saint Louis wakasawazisha bao hilo dakika ya pili kati ya nne za nyongeza baada ya kutimia dakika 90 za kawaida kupitia kwa Nahodha wake, Betrand Esther aliyefunga kwa kichwa baada ya mabeki wa Yanga kuzembea kuokoa mpira wa juu.
  Kwa matokeo hayo, Yanga itakutana na Township Rollers ya Botswana iliyoitoa El Merreikh ya Sudan.
  Pole Nahodha Cannavaro. Mungu ampumzishe kwa amani kipenzi chako. Na Mungu akujaalie moyo wa ustahmilifu katika kipindi hiki kigumu kwako na familia yako.  
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: NAHODHA YANGA, NADIR HAROUB 'CANNAVARO' AFIWA NA MWANAWE MUHIMBILI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top