• HABARI MPYA

  Jumapili, Februari 25, 2018

  MAJI MAJI YASIMAMISHA WACHEZAJI WATANO IKIIVAA YANGA SC LEO SONGEA

  Na Mwandishi Wetu, SONGEA 
  WAKATI leo inamenyana na Yanga SC katika mchezo wa hatua ya 16 Bora michuano ya Azam Sports Federation Cup (ASFC), uongozi wa Maji Maji FC ya Songea umewasimamisha wachezaji wake watano kwa tuhuma za utovu wa nidhamu.
  Kocha wa Maji Maji, Habib Kondo amewataja wachezaji waliosimamishwa ni Andrew Ntala, Sadik Galacha, Paul Maona, Alex Kondo na Six Mwasegaga.
  Kondo alisema kwamba wachezaji wote hao wamesimamishwa kwa kosa la kugoma kufanya mazoezi, huku pia wakiwachochea wachezaji wengine kufanya hivyo.
  Lakini taarifa zinasema wachezaji hao waligoma ili kushinikiza kulipwa stahiki zao mbalimbali, ikiwemo malimbikizo ya mishahara, fedha za usajili na posho.
  Kondo amesema kuondoka kwa watano kunafanya idadi ya wachezaji wa kikosi cha kwanza walioondoka Maji Maji kufika saba, baada ya kuondoka kwa Suleiman Kassim ‘Selembe’ na Kenneddy Kipepe.
  Lakini Kondo amesema kwamba tayari amechukua wachezaji kutoka timu ya vijana chini ya umri wa miaka 20 kuziba nafasi hizo na anaamini watafanya vizuri.
  “Ukweli ni kwamba wachezaji walioondoka walikuwa wa kikosi cha kwanza kwa hiyo ni pigo katika timu, lakini kwa kuwa tupo vitani tutaingia kupambana na hawa hawa tulionao,”alisema Kondo. 
  Yanga SC iliwasili Songea mapema jana kwa ndege, ikiwa ni siku moja tangu irejee Dar es Salaam Alhamisi usiku kutoka Mahe, Shelisheli ambako Jumatano ilikata tiketi ya kwenda Raundi ya Kwanza ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika licha ya sare ya 1-1 na wenyeji, Saint Louis Suns United katika mchezo wa marudiano wa Raundi ya Awali Uwanja wa Linite.
  Mabingwa hao wa Tanzania wamesonga mbele kwa ushindi wa jumla wa 2-1 baada ya Februari 10 kushinda 1-0 pia Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, bao pekee la kiungo Juma Mahadhi aliyekosekana uwanjani Jumatano kwa sababu ya homa.
  Kwa kuitoa St Louis, Yanga itakutana na Township Rollers ya Botswana katika Raundi ya Kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika, ambayo nayo iliitoa El Merreikh ya Sudan, mechi ya kwanza ikichezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam Machi 6 kabla ya kwenda Gaborone kwa mchezo wa marudiano, Machi 17.
  Mbali na Maji Maji na Yanga, mechi nyingine za ASFC leo ni Buseresere FC na Mtibwa Sugar Uwanja wa Nyamagana mjini Mwanza na JKT Tanzania watakaomenyana na Ndanda FC Uwanja wa Azam Complex Chamazi, Dar es Salaam.
  Mechi za 16 Bora ya ASFC zitakamilishwa Jumatatu ya Februari 26, Kiluvya United wakiwa wenyeji wa Tanzania Prisons Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani na Stand United watakuwa wenyeji wa Dodoma FC Uwanja wa Kambarage, Shinyanga.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: MAJI MAJI YASIMAMISHA WACHEZAJI WATANO IKIIVAA YANGA SC LEO SONGEA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top