• HABARI MPYA

  Wednesday, February 21, 2018

  NI KUFA NA KUPONA YANGA LEO SHELISHELI…MUNGU AWABARIKI WAVUKE HATUA HII

  Na Mwandishi Wetu, VICTORIA
  YANGA SC leo wanateremka Uwanja wa Linite mjini Victoria, Shelisheli kumenyana na wenyeji, Saint Louis Suns United katika mchezo wa marudiano Raundi ya Awali Ligi ya Mabingwa Afrika.
  Timu hiyo ya kocha George Lwandamina, anayesaidiwa na Mzambia mwenzake, Noel Mwandila na wazalendo, Nsajigwa Shadrack na Juma Pondamali, kocha wa makipa inatakiwa kuulinda ushindi wake mwembamba wa 1-0 katika mchezo wa kwanza Dar es Salaam siku 10 zilizopita.
  Mchezo wa leo ambao utarushwa moja kwa moja na Azam TV kupitia chaneli ya Azam Sports Two, unatarajiwa kuanza Saa 11:30 jioni kwa saa za Shelisheli na Saa 10:30 kwa Saa za Tanzania. 
  Kila la heri Yanga SC katika mchezo na wenyeji, Saint Louis Suns United leo Shelisheli 

  Kikosi cha Yanga kiliwasili Victoria Jumapili jioni na baada ya mazoezi ya siku mbili mjini humo kwenye hali ya hewa nzito, kipo tayari kupigania tiketi ya kusonga mbele Ligi ya Mabingwa.
  Yanga SC inaingia kwenye mchezo wa leo bila wachezaji wake kadhaa nyota ambao ni majeruhi na mbaya zaidi haitakuwa na mshambuliaji hata mmoja.
  Mrundi Amissi Tambwe na Mzimbabwe Donald Ngoma wote ni majeruhi wa muda mrefu, wakati kiungo Mzambia ambaye amekuwa akitumika mshambuliaji siku za karibuni naye amebaki Dar es Salaam kwa sababu ya maumivu.
  Hapana shaka Lwandamina anaweza kuwatumia viungo wengine, Ibrahim Ajib, Pius Buswita au Juma Mahadhi katika eneo la washambuliaji leo.
  Lakini hadi jana usiku, Mahadhi aliye katika msimu wake wa pili Yanga tangu asajiliwe kutoka Coastal Union ya Tanga alikuwa anasumbuliwa na homa, hivyo uwezekano wa yeye kucheza ni mdogo.    
  Mshindi wa jumla wa mchezo wa leo atakutana na mshindi wa jumla kati ya El Merreikh ya Sudan na Township Rollers ya Botswana. Katika mchezo wa kwanza, Township Rollers ilishinda 3-0 nyumbani.
  Mtaji wa ushindi wa 1-0 nyumbani ni mdogo – maana yake, Yanga wanaingia katika mtihani mgumu leo na wanahitaji kupigana kufa na kupona ili kusonga mbele. Kila la heri Yanga SC. Mungu awabariki wavuke hatua hii. Amin. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: NI KUFA NA KUPONA YANGA LEO SHELISHELI…MUNGU AWABARIKI WAVUKE HATUA HII Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top