• HABARI MPYA

  Alhamisi, Februari 22, 2018

  MTIBWA SUGAR WAPANIA KUBEBA KOMBE LA AZAM SPORTS FEDERATION

  Na Mwandishi Wetu, MOROGORO
  TIMU ya Mtibwa Sugar imeweka dhamira ya kutwaa taji la Azam Sports Federation Cup (ASFC) ili kurudisha heshima yake iliyopotea kwa sasa kwenye soka ya Tanzania.
  Kocha wa Mtibwa Sugar, Zuberi Katwila amesema kwamba wanataka kurudi kwenye michuano ya Afrika na katika kuhakikisha wanatimiza azma hiyo lazima wapigane watwae Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
  Katwila amesema kwamba kuanzia sasa wanakwenda kwenye mchezo wa hatua ya 16 Bora ya michuano hiyo inayodhaminiwa na Azam TV wakiwa na lengo moja tu, kushinda na kwenda Robo Fainali. 
  Mtibwa wanatarajiwa kuwa wageni wa Buseresere FC Jumapili Uwanja wa Nyamagana mjini Mwanza katika mchezo wa 16 Bora ya Azam Sports Federation Cup na kikosi kimeondoka leo kwenda mjini humo.
  Kocha wa Mtibwa Sugar, Zuberi Katwila amepania kuirudisha timu kwenye michuano ya Afrika 

  Katwila amesema kwamba wanatarajia ushindani mkali kutoka kwa Buseresere FC ambayo pamoja na kuwa Ligi Daraja la Pili, lakini iliitoa timu nyingine ya Ligi Kuu, Kagera Sugar.
  “Buseresere si timu ya timu kubeza, kama wameweza kuitoa Kagera Sugar basi wanaweza kuitoa timu yoyote. Ndiyo maana sisi tumejiandaa kikamilifu kwa ajili ya mchezo huu,”amesema Katwila.
  Hatua ya 16 ya ASFC ilianza jana kwa Njombe FC kuwa timu ya kwanza kuingia Robo Fainali kwa ushindi wa penalti 6-5 kufuatia sare ya 1-1 na Mbao FC ya Mwanza ndani ya dakika 90 Uwanja wa Saba Saba mjini Njombe.
  Sasa timu zote zilizocheza fainali ya ASFC Mei 27, mwaka jana Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma zinaipa mgongo michuano hiyo hata kabla ya hatua ya Robo Fainali.
  Hiyo ni baada ya Simba, waliotwaa taji hilo kwa ushindi wa 2-1 kutolewa pia Desemba 22 kwa penalti 4-3, baada ya sare ya 1-1 ndani ya dakika 90 na timu ya Daraja la Pili, Green Worriors ya Mwenge, Dar es Salaam inayomilikiwa na Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) katika hatua ya 64 Bora.
  Hatua ya 16 Bora ya ASFC itaendelea kesho wakati Singida United watakapowakaribisha Polisi Tanzania Uwanja wa Namfua mjini Singida na KMC watamenyana na Azam FC Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
  Mbali na Buseresere na Mtibwa Sugar, mechi nyingine za Jumapili ni Maji Maji FC watakaokuwa wenyeji wa Yanga SC Uwanja wa Maji Maji mjini Songea na JKT Tanzania watamenyana na Ndanda FC Uwanja wa Azam Complex Chamazi, Dar es Salaam.
  Mechi za 16 Bora ya ASFC zitakamilishwa Jumatatu ya Februari 26, Kiluvya United wakiwa wenyeji wa Tanzania Prisons Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani na Stand United watakuwa wenyeji wa Dodoma FC Uwanja wa Kambarage, Shinyanga.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: MTIBWA SUGAR WAPANIA KUBEBA KOMBE LA AZAM SPORTS FEDERATION Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top