• HABARI MPYA

  Jumatatu, Februari 26, 2018

  SIMBA SC WAIKARIBISHA MBAO FC LIGI KUU UWANJA WA TAIFA LEO

  REKODI YA SIMBA SC NA MBAO FC:
                        P W D GF GA GD Pts
  Simba SC      4 3 1 8 5 3 10
  Mbao FC       4 - 1 5 8 -3 1
  Alhamisi Septemba 21 2017
  Mbao FC 2-2 Simba SC (Ligi Kuu Kirumba, Mwanza)
  Jumamosi Mei 27, 2017
  Simba SC 2-1 Mbao FC (Fainali ASFC, Jamhuri, Dodoma)
  Jumatatu Aprili 10, 2017
  Mbao FC 2-3 Simba SC (Ligi Kuu, Kirumba, Mwanza)
  Alhamisi Oktoba 20, 2016
  Simba SC 1-0 Mbao FC (Ligi Kuu, Uhuru, Dar es Salaam)
  Kutoka kulia Emmanuel Okwi, Said Ndemla na John Bocco wanatarajiwa kuiongoza Simba SC dhidi ya Mbao FC leo

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  LIGI Kuu ya Vodacom Tanzania Bara inatarajiwa kuendelea leo kwa mchezo kati ya Simba SC na Mbao FC ya Mwanza Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
  Hiyo itakuwa mara ya tano kwa timu hizo kukutana, tangu Mbao FC inayofundishwa na kocha Mrundi, Ettienne Ndayiragijje ipande Ligi Kuu msimu uliopita na timu hiyo ya Mwanza haijawahi kupata ushindi dhidi ya vigogo wa soka nchini, Simba SC.
  Mbao FC wanaingia kwenye mchezo wa leo wakitoka kuondolewa kwenye michuano ya Azam Sports Federation Cup (ASFC) Hatua ya 16 Bora na Njombe Mji FC wakifungwa kwa penalti 6-5 kufuatia sare ya 1-1 Februari 21 mjini Njombe.
  Simba SC wanaingia kwenye mechi ya leo wakitoka kusonga mbele kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya ushindi wa 1-0 Februari 20 dhidi ya wenyeji, Gendarmerie Tnare mjini Djibouti City, bao pekee la Mganda, Emmanuel Okwi.
  Matokeo hayo yaliifanya Simba SC isonge mbele kwa ushindi wa jumla wa 5-0 baada ya kushinda 4-0 kwenye mchezo wa kwanza mjini Dar es Salaam.
  Lakini katika mechi zao zilizopita za Ligi Kuu, wote walitoa sare, Mbao FC wakitoka 0-0 na Mtibwa Sugar Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza Jumapili ya Februari 11 na Simba SC wakitoka 2-2 na wenyeji, Mwadui FC Alhamisi ya Februari 15 Uwanja wa Kambarage, Shinyanga.
  Simba SC inayofundishwa na kocha Mfaransa, Pierre Lechantre anayesaidiwa na Mrundi, Masoud Juma, Mtunisia, Mohammed Aymen Hbibi kocha wa mazoezi ya viungo na mzalendo Muharami Mohammed ‘Shilton’, kocha wa makipa ndiyo vinara wa Ligi Kuu kwa sasa wakiwa na pointi zao 42 baada ya kucheza mechi 18.
  Wanafuatiwa kwa mbali kidogo na mabingwa watetezi, Yanga SC wenye pointi 37 za mechi 18 pia, wakati Singida United yenye pointi 36 za mechi 19 ni ya tatu, Azam FC yenye pointi 35 za mechi 19 ni ya nne na Tanzania Prisons inashika nafasi ya tano kwa pointi zake 29 za mechi 19, wakati Mbao FC yenye pointi 19 za mechi 18 ni ya 11 katika Ligi Kuu ya timu 16. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: SIMBA SC WAIKARIBISHA MBAO FC LIGI KUU UWANJA WA TAIFA LEO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top