• HABARI MPYA

  Jumatano, Desemba 27, 2017

  SIMBA SC KUIFUATA NDANDA ‘JOGOO LA KWANZA’ TU KESHO

  Na Princess Asia, DAR ES SALAAM
  WAKATI jogoo la kwanza linawika kesho alfajiri, vinara wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Simba SC wanatarajiwa kuanza safari mjini Dar es Salaam kwenda Mtwara kwa ajili ya mchezo dhidi ya Ndanda FC Jumamosi Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara.
  Wachezaji wote wanatarajiwa kuwa safarini kesho kwa ajili ya mchezo huo, ukiondoa kipa Said Mohammed ‘Nduda’ na mabeki Shomary Kapombe na Salim Mbonde ambao ni majeruhi.
  Simba ipo kambini katika hoteli ya SeaScape, Kunduchi mjini Dar es Salaam tangu jana baada ya mapumziko ya siku mbili kwa ajili ya sikukuu ya Krisimasi.
  Simba SC wataondoka kesho wakiwa na kumbukumbu mbaya ya kuvuliwa mapema ubingwa wa Azam Sports Federation Cup (ASFC) baada ya kuchapwa kwa penalti 4-3 na Green Warriors ya Mwenge kufuatia sare ya 1-1 ndani ya dakika 90. 
  Lakini wanakwenda Mtwara wakiwa wanaongoza Ligi Kuu kwa pointi zao 23 sawa na Azam FC, wakiwazidi kwa pointi mbili mabingwa watetezi, Yanga SC baada ya timu zote kucheza mechi 11.
  Kwa ujumla, Ligi Kuu inatarajiwa kuendelea Ijumaa baada ya mapumziko ya wiki tatu kupisha michuano ya CECAFA Challenge iliyomalizika nchini Kenya wiki iliyopita kwa wenyeji, Harambee Stars kuwa mabingwa wakiwafunga Zanzibar katika fainali.
  Ijumaa Azam FC watakuwa wenyeji wa Stand United Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam kuanzia Saa 1:00 usiku na Jumamosi kutakuwa na mechi tatu, Lipuli na Tanzania Prisons Uwanja wa Samora, Iringa kuanzia Saa 8:00 mchana, Mtibwa Sugar na Maji Maji Uwanja wa Manungu, Turiani, Morogoro na Ndanda FC na Simba SC Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara zote zikianza saa 10:00 jioni.
  Jumapili, mabingwa watetezi, Yanga watakuwa wageni wa Mbao FC Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza saa 10:00 jioni na Njombe Mji FC wataikaribisha Singida United kuanzia saa 8:00 mchana Uwanja wa Saba Saba, Njombe.
  Mechi za kukamilisha mzunguko wa 12 zitachezwa mwaka mpya, Januari 1 Mbeya City wakiikaribisha Kagera Sugar Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya  na Mwadui wakiikaribisha Ruvu Shooting zote kuanzia saa 10:00 jioni.
  Baada ya mechi hizo, Ligi Kuu itasimama tena kupisha mechi za Kombe la Mapinduzi visiwani Zanzibar na raundi ya tatu ya Azam Sports Federation Cup (ASFC) itakayochezwa kati ya Januari 5 na 7 mwakani kabla ya kuingia kwenye mzunguko wa 13 wa ligi kuanzia Januari 13 na 17, 2018.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: SIMBA SC KUIFUATA NDANDA ‘JOGOO LA KWANZA’ TU KESHO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top