• HABARI MPYA

  Ijumaa, Desemba 29, 2017

  ARTHUR AFUNGA ‘BAO TAMU’ AZAM FC YAUA 3-0 NA KUPAA KILELENI LIGI KUU

  Na Salma Suleiman, DAR ES SALAAM
  AZAM FC imesogea juu kabisa ya msimamo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara baada ya ushindi wa 3-0 dhidi ya Stand United ya Shinyanga usiku huu Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
  Ushindi huo unaifanya Azam ifikishe pointi 26 baada ya kucheza mechi 12, ikiwazidi kwa pointi tatu vinara wa muda mrefu msimu huu, SImba SC na pointi tano mabingwa watetezi, Yanga SC ambao wote wamecheza mechi 11. 
  Simba kesho watacheza mechi ya 12 ugenini kwa Ndanda FC Uwanja wa Nanganwada Sijaona, Mtwara wakati watani wao, Yanga watacheza Jumapili Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza na wenyeji, Mbao FC.
  Katika mchezo  wa leo, Azam ilipata bao lake la kwanza dakika ya 21, mfungaji kiungo Salmin Hoza aliye katika msimu wake wa kwanza Chamazi baada ya kusajiliwa kutoka Mbao FC ya Mwanza, akipiga shuti la umbali wa mita 20 baada ya kutengewa pasi na kiungo wa ulinzi, Mcameroon, Stepgan Kingue Mpondo.
  Katika 45 za kipindi hicho Azam walionekana kuutawala mchezo licha ya kuwa Stand walikuwa wanaendana na kasi yao kiuchezaji na kuonyesha kujaribu kufika langoni kwao mara kadhaa.
  Azam FC ambayo leo kocha Mromania, Aristica Cioaba alikuwa jukwaani baada ya kufungiwa kwa utovu wa nidhamu, ilifanya mabadiliko dakika ya 32 ikimtoa chipukizi Iddi Kipangwile na kumuingiza mshambuliaji mpya, Mghana, Bernard Arthur.
  Mabadiliko hayo kwa Azam yalionekana kuiongezea spidi safu ya ushambuliaji ya Azam, lakini kutokana na umakini wa kipa wa Stand United, Frank Muwonge waliishia kukosa mabao ya wazi.
  Refa Emmanuel Mwandembwa kutoka Arusha alimuonyesha kadi ya njano Hoza dakika ya 41 kwa kumchezea rafu Juvenaris Pastory.
  Wakati huo huo, Arthur alifumua shuti zuri lililokwenda nje sentimita chache baada ya pasi nzuri ya Mghana mwenzake, winga Enock Atta Agyei.
  Kipindi cha pili nyota ya Azam FC iliendelea kung’ara wakafanikiwa kuongeza mabao mawili, dakika ya 64 mfungaji Arthur akimalizia pasi ya Yahya Zayed kwa kumpiga chenga kipa, Frank Muwonge na dakika ya 78, Bruce Kangwa akawapangua mabeki wa Stand United na kuingia ndani ya boksi kabla ya kufumua shuti lililompita kipa Mganda.
  Kikosi cha Azam FC kilikuwa; Razack Abalora, Himid Mao, Bruce Kangwa, Yakubu Mohamed, Aggrey Morris, Stephan Kingue/Salum Abubakar ‘Sure Boy’ dk62, Idd Kipangwile/Bernard Arthur dk32, Salmin Hoza, Yahya Zayed, Enock Atta Agyei/Shaaban Iddi dk81 na Joseph Mahundi
  Stand United; Frank Mwonge, Aaron Lulambo, Miraji Maka, Mayanga Vitaris, Erick Mulilo, Juventus Pastory Blais Bigirimana, Landry Ndikumana, Jisend Maganda, Tarick Seif na Frank Zakaria/Sixtus Sabilo dk74.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: ARTHUR AFUNGA ‘BAO TAMU’ AZAM FC YAUA 3-0 NA KUPAA KILELENI LIGI KUU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top