• HABARI MPYA

  Ijumaa, Desemba 22, 2017

  SINGIDA UNITED YATEMA MZIMBABWE, YASAJILI BEKI WA KATI WA BLACK STARS YA GHANA

  Na Salma Suleiman, DAR ES SALAAM
  TIMU ya Singida imeimarisha safu yake ya ulinzi kwa kumsajili beki wa Mghana, Malik Antri ambaye alikuwemo kwenye kikosi cha timu ya taifa ya wachezaji wa nyumbani kwa ajili ya michuano ya CHAN.
  Taarifa ya Mkurugenzi wa Singida United, Sanga Festo imesema kwamba Antri amekwishawasili nchini tayari kuitumikia Singida United ambayo inapambana kuhakikisha inatwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara katika msimu wa kwanza tangu wapande.
  Sanga Festo amesema kwamba Antri anachukua nafasi ya Elisha Muroiwa aliyerejea kwao Zimbabwe kufuatia matatizo ya kifamilia yanayomsumbua.
  Huyu ndiye beki mpya Mghana wa Singida United, Malik Antri aliyekuwemo kwenye kikosi cha CHAN cha Black Stars

  Na Antri anakuwa mchezaji wa nane kusajiliwa dirisha dogo Singida United, baada ya washambuliaji Daniel Lyanga kutoka Fanja ya Oman, Kambale Salita 'Papy Kambale' kutoka Etincelles ya Rwanda na Lubinda Mundia kwa mkopo kutoka Res Arrows ya Zambia.
  Wengine ni chipukizi Issa Makamba, Assad Juma, Ally Ng’azi na Mohamed Abdallah waliokuwa kwenye kikosi cha timu ya taifa ya vijana ya Tanzania chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Boys kilichoshiriki fainali za U-17 Afrika nchini Gabon Mei mwaka huu.
  Singida United inayofundishwa na kocha wa zamani wa Yanga, Mholanzi Hans van der Pluijm kwa sasa inashika nafasi ya nne kwenye msimamo wa Ligi Kuu ikiwa na pointi 20 baada ya kucheza mechi 11.
  Inazidiwa pointi tatu na Simba na Azam na mbili na mabingwa watetezi, Yanga.  Na baada ya mapumziko ya wiki tatu kupisha michuano ya CECAFA Challenge iliyofikia tamati Jumapili nchini Kenya, Ligi Kuu itarejea mwishoni mwa mwezi huu na Singida itawafuata Njombe Mji FC Desemba 31 Uwanja wa Saba Saba huko Njombe, mchezo utakaoanza Saa 8:00 mchana.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: SINGIDA UNITED YATEMA MZIMBABWE, YASAJILI BEKI WA KATI WA BLACK STARS YA GHANA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top