• HABARI MPYA

  Jumapili, Desemba 31, 2017

  YANGA ‘ROJO ROJO’ KWA MBAO…YAPIGWA 2-0 KIRUMBA HADI AIBU

  Na Mwandishi Wetu, MWANZA
  MBAO FC imeendeleza ubabe mbele ya Yanga baada ya ushindi wa mabao 2-0 leo Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza.
  Shujaa wa Mbao FC alikuwa ni mshambuliaji chipukizi, Habib Hajji Kiyombo aliyefunga mabao yote hayo dakika za 53 na 68. 
  Na kwa ushindi huo,  Mbao FC inafikisha pointi 14 baada ya kucheza mechi 12 na kupanda hadi nafasi ya saba kutoka ya nane.
  Yanga wao wanajitoa kwenye tatu bora, wakibaki na pointi zao 21 baada ya mechi 12 za msimu wa 2017-2018, wakiwa nyuma ya Singida United pointi 23 na Azam na Simba zenye pointi 26 kila moja.
  Habib Hajji Kiyombo amefunga mabao yote leo Mbao FC ikiichapa Yanga 2-0 

  Kiyombo  alifunga bao la kwanza dakika ya 53 kwa shuti la umbali wa mita 25 baada ya kuwatoka wachezaji wa Yanga na la pili dakika ya 68 kwa shuti pia, safari hii ndani ya boksi baada ya kupokea pasi ya Boniphace Maganga.
  Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Suleiman Kinugani aliyesaidiwa na Jesse Erasmo wote wa Morogoro na Godfrey Kihwili wa Arusha, kipindi cha kwanza timu zote zilishambuliana kwa zamu
  Beki Abdallah Hajji Shaibu ‘Ninja’ akicheza mechi yake ya kwanza ya Ligi Kuu msimu huu tangu asajiliwe Yanga msimu huu alicheza vizuri kwa kujiamini na ustadi wa hali ya juu dhidi ya washambuliaji chipukizi, wepesi na mahiri wa Mbao akina James Msuva, Habib Kiyombo na Emmanuel Mvuyekure.
  Mbao walikuwa wakishambulia moja kwa moja kipindi cha kwanza na zadi wakipitia eneo la katikati ya Uwanja kupeleka mashambulizi yao, lakini Yanga walikuwa wakipitishia mipira pembeni zaidi.
  Kipindi cha pili, Mbao FC wakarudi na maarifa mapya na kufanikiwa kupata mabao yao mawili ndani ya robo saa.  
  Refa Kinugani akampandisha jukwaani kocha wa Mbao FC, Ettienne Ndayiragijje dakika ya 75 baada ya kupishana kauli na refa wa akiba, Joseph Masija wa Mwanza.
  Dakika moja baadaye, Mbao wakapata pigo tena baada ya beki wao, David Mwasa kuonyeshwa kadi ya pili ya njano na kutolewa kwa kadi nyekundu kwa kumchezea rafu Tambwe.
  Pamoja na kubaki pungufu na bila kocha wake mkuu pia, Mbao FC wakacheza vizuri na kumalizia mchezo kwa ushindi wa 2-0. 
  Huo unakuwa mchezo wa tatu mfululizo Yanga inafungwa Mbao FC, nyingine zote mbili hapo hapo Kirumba mjini Mwanza 1-0 mara zote, kwanza katika michuano ya Azam Sports Federation Cup (ASFC) Aprili 30 na baadaye katika Ligi Kuu Mei 20 baada ya mabingwa hao wa Ligi Kuu kushinda 3-0 kwenye mchezo wa kwanza wa ligi Oktoba 29, mwaka 2016 Dar es Salaam. 
  Kikosi cha Mbao FC leo kilikuwa; Ivan Kugumbandiye, Vincent Philipo, Amos Charles, David Mwasa, Yusuph Ndikumana, Ibrahim Njohole, George Sangija, James Msuva/Boniphace Maganga dk64, Habib Haji, Emmanuel Mvuyekure na Abubakar Mfaume.
  Yanga SC; Youthe Rostande, Juma Abdul/Hassan Kessy dk80, Gardiel Michael, Andrew Vincent ‘Dante’, Abdallah Shaibu ‘Ninja’, Pato Ngonyani, Pius Buswita, Papy Kabamba Tshishimbi/Yusuph Mhilu dk72, Amissi Tambwe, Raphael Daudi na Emmanuel Martin/Geoffrey Mwashiuya dk58. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: YANGA ‘ROJO ROJO’ KWA MBAO…YAPIGWA 2-0 KIRUMBA HADI AIBU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top