• HABARI MPYA

  Ijumaa, Desemba 22, 2017

  POLISI WAMCHUNGUZA GUARDIOLA KWA UCHOCHEZI HISPANIA

  KOCHA wa Manchester City, Pep Guardiola ametajwa kwenye ripoti ya Polisi kwamba anachunguzwa juu ya harakati za kupigania Uhuru wa Katalunya kujitenga kutoka Hispania.
  Wanaharakati Jordi Sanchez na Jordi Cuixart waliwekwa rumande Oktoba mwaka huu kwa kuongoza harakati hizo, jambo ambalo ni kuvunja sheria za Hispania. 
  Wamekuwa wakichunguzwa kwa mienendo yao na watu wanaoshirikiana nao na taarifa zinasema Guardiola anahusika na anaweza kupandishwa Mahakama Kuu mbele ya Jaji Pablo Llaren.  
  Guardiola anafahamika wazi kama anaunga mkono kampeni za Katalunya kuwa nchi inayojitegemea kwa kujitenga kutoka Serikali ya Hispania yenye makao yake makuu Madrid.

  Kocha wa Manchester City, Pep Guardiola akiuhutubia umati wa maelfu ya watu PICHA ZAIDI GONGA HAPA

  Kocha huyo wa City alihudhuria mbio maalum za harakati hizo, 'Pro-independence Rally' mjini Barcelona hivi karibuni pamoja na Carles Puigdemont, Rais wa Serikali ya Katalunya na watu wengine 10,000.   
  Aliuambia umati kwamba atapiga kura ya Uhuru Oktoba 1 'hata kama nchi ya Hispania haitataka hilo'.
  Hata hivyo, kura hizo hazikutambuliwa na Madrid, Polisi wa Hispania wameanza uchunguzi juu ya mtu huyo maarufu ambaye alithubutu kutoa maoni yake mbele ya umma.
  Taarifa ya Polisi, iliyonukuliwa kwenye gazeti la Kispaniola la El Nacional, ilisema kwamba 'kampeni ziliongozwa na Josep Guardiola na alithubutu kuwaambia wafuasi wote wapiganie Uhuru'.  
  Zoezi hilo lilifanyika Oktoba 1 na wasiasa wa  Pro-Independence, Oriol Junqueras na Joaquim Forn na wanaharakati Jordi Sanchez na Jordi Cuixart mara moja waliswekwa rumande.
  Rais wa Katalunya, Carles Puigdemont alikimbilia mji wa Brussels nchini Ubelgiji na ameambiwa atakamatwa pia akirejea Hispania.
  Guardiola amekuwa akivaa lebo ya njano kama sehemu ya kampeni zake za kutaka wanasiasa na wanaharakati waliokamatwa waachiwe na hivi karibuni alisema: "Kama UEFA ama FIFA, au Ligi Kuu (England) wanataka kuniadhibu mimi kwa kuvaa lebo ya njano wafanye hivyo. Ninanvaa hii kwa ajili ya watu wawili ambao wapo jela kwa sababu ya kutetea haki ya kupiga kura,".  
  Malalamiko ya kuvaa lebo ya kuunga mkono harakati za Katalunya kujitenga yaliibuliwana kocha wa Manchester United, Jose Mourinho hivi karibuni.
  Mourinho alihoji kwa nini mpinzani wake huyo wa muda mrefu anaruhusiwa kuvaa lebo hiyo na akashauri mambo ya kisiasa yasiingizwe kwenye michezo. 
  UEFA imekwishabadili sheria zake msimu huu na sasa ujumbe wa ishara tu ndiyo unaruhusiwa – ambayo inatumika pia na FA - na kwa maana hiyo Guardiola alikuwa huru kuvaa lebo hiyo.    
  Katalunya walitarajiwa kupiga kura jana kuchagua uongozi mpya wa Serikali yao, zoezi ambalo linatarajiwa kuleta mgawanyiko zaidi.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: POLISI WAMCHUNGUZA GUARDIOLA KWA UCHOCHEZI HISPANIA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top