• HABARI MPYA

    Saturday, December 30, 2017

    NSAJIGWA: JEURI YA MBAO TUTAIMALIZA KESHO KIRUMBA

    Na Abdallah Chaus, MWANZA 
    KOCHA Msaidizi wa mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Nsajigwa Shadrack ‘Fuso’ amesema kwamba hana hofu yoyote kuelekea mchezo wa kesho wa ligi hiyo dhidi ya wenyeji, Mbao FC Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza.
    Nsajigwa, beki na Nahodha wa zamani wa klabu hiyo ya Dar es Salaam, ameyasema hayo leo asubuhi katika mahojiano maalum na Bin Zubeiry Sports – Online wakati wa mazoezi ya mwisho keuelekea mchezo wa kesho.
    “Sina hofu na Mbao katika mchezo wa kesho, kwani naamini kikosi changu kiko fiti majeruhi wote tumewaacha Dar es Salaam, hapa tumekuja kufanya kazi na Mungu akituamsha salama tutaifanya hiyo kazi,”amesema.
    Nsajigwa Shadrack (kushoto) amesema hawahofii Mbao FC kuelekea mchezo wa Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza

    Akiwazungumzia wapinzani wake, Nsajigwa amesema kwamba anawaheshimu Mbao FC, kwani ni timu nzuri na ina wachezaji vijana na wenye uwezo mkubwa, huku akimpa heshima kocha wa timu hiyo, Ettienne Ndayiragije kwa kuweza kufanya vyema katika msimu uliopita.
    Aidha, Nsajigwa amesema kurejea kwa mshambuliaji wao aliyekuwa majeruhi kwa muda mrefu, Mrundi Amisi Tambwe ni faraja kwake, kwani mkali huyo wa mabao anakuja kuiongezea nguvu timu. “Tunanamuombea kwa Mungu (Tambwe) aamke salama na akafanye kazi,”amesema.
    Yanga itaingia kwenye mchezo wa kesho ikiwa na kumbukumbu ya kufungwa 1-0 mara mbili mfululizo na Mbao Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza msimu uliopita, kwanza katika michuano ya Azam Sports Federation Cup (ASFC) Aprili 30 na baadaye katika Ligi Kuu Mei 20 baada ya mabingwa hao wa Ligi Kuu kushinda 3-0 kwenye mchezo wa kwanza wa ligi Oktoba 29, mwaka 2016 Dar es Salaam.
    Michezo mingine ya Ligi Kuu kesho, Njombe Mji FC watawakaribisha Singida United Uwanja wa Saba Saba mjini Njombe kuanzia Saa 8:00 mchana, wakati Jumatatu Mbeya City watawakaribisha Kagera Sugar Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya na Mwadui FC watakuwa wenyeji wa Ruvu Shooting Uwanja wa Mwadui Compex, Kishapu.
    Baada ya raundi ya 12, Ligi Kuu ya Vodacom itapisha mechi za Kombe la Mapinduzi na raundi ya tatu ya Kombe la Shirikisho la Azam Sports itakayochezwa kati ya Januari 5 na 7 mwakani kabla ya kuingia raundi ya 13 itakayofanyika kati ya Januari 13 na 17, 2018.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: NSAJIGWA: JEURI YA MBAO TUTAIMALIZA KESHO KIRUMBA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top