• HABARI MPYA

    Tuesday, December 19, 2017

    AZAM FC YAWACHAPA POLISI TANZANIA 3-1 CHAMAZI

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    TIMU ya Azam FC imemaliza programu ya mechi za kirafiki kwa kuinyuka Polisi Tanzania mabao 3-1 katika mchezo wa kirafiki uliofanyika Uwanja wa Azam Complex leo usiku.
    Shujaa za Azam FC katika mchezo huo, alikuwa mshambuliaji kinda aliyepandishwa, Paul Peter, aliyeingia dakika ya 50 kuchukua nafasi ya Bernard Arthur, baada ya kufunga mabao mawili ya kiufundi  akitumia dakika sita tu tokea aingie la kwanza dakika ya 53 na la pili 56.
    Mabao hayo yalifuta uongozi wa Polisi Tanzania waliojipatia bao kipindi cha kwanza, huku mshambuliaji Wazir Junior aliyeingia dakika ya 80 kuchukua nafasi ya Yahya Zayd, akihitimisha ushindi mnono wa Azam FC baada ya kutupia bao la tatu dakika ya 81 akimalizia krosi ya chini ya beki wa kulia Swaleh Abdallah.
    Azam FC ingeweza kujipatia mabao zaidi kama nahodha wake, Himid Mao ‘Ninja’, angefunga mkwaju wa penalti dakika ya 77, lakini mpira aliopiga uligonga mwamba wa pembeni na kuokolewa na mabeki, adhabu ya penalti ikipatikana baada ya Peter kuangushwa ndani ya eneo la hatari.
    Mchezo huo uliokuwa mkali na wa aina yake, ilishuhudiwa dakika ya 68 Azam FC ikipata pigo baada ya beki wake, Daniel Amoah kuumia mguu baada ya kuanguka kwenye eneo la nje ya uwanja akiwa kwenye harakati za kuokoa shambulizi lililokuwa likielekezwa langoni kwake.
    Mechi hiyo ya kirafiki ilikuwa ni ya nne katika kipindi hiki cha mapumziko ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL), awali iiitangulia kutoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Friends Rangers kabla ya kuzichapa Mvuvumwa (8-1) na Villa Squad ya Kinondoni (7-1).
    Benchi la ufundi la Azam FC limezitumia mechi hizo kama sehemu ya maandalizi kuelekea mchezo wa raundi ya 64 ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) dhidi ya Area C United utakaofanyika Uwanja wa Azam Complex Jumamosi hii saa 10.00 jioni.
    Kikosi cha Azam FC leo; Razack Abalora, Himid Mao (C)/Swaleh Abdallah dk 79, Bruce Kangwa/Abdul Omary dk 77, Agrey Moris/Yakubu Moahmmed dk 86, Daniel Amoah/Oscar Masai dk 68, Stephan Kingue/Frank Domayo dk 36/Ramadhan Mohamed dk 90, Joseph Mahundi/Idd Kipagwile dk 36, Salmin Hoza/Salum Abubakar dk 46, Yahya Zayd/Wazir Junior dk 80, Bernard Arthur/Paul Peter dk 50, Enock Atta/Masoud Abdallah dk 61
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: AZAM FC YAWACHAPA POLISI TANZANIA 3-1 CHAMAZI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top