• HABARI MPYA

  Alhamisi, Desemba 21, 2017

  TANZANIA ‘MWENDO MDUNDO’ KUELEKEA CHINI, YAPOROMOKA TENA FIFA

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  SOKA ya Tanzania imezidi kudidimia baada ya kuporomoka kwa nafasi tano zaidi kwenye viwango vya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) kwa mwezi Novemba.
  Taarifa ya FIFA leo juu ya viwango vya Novemba 2017, inaonyesha Tanzania sasa inashika nafasi ya 147 kutoka ya 142 mwezi Oktoba, wakati Uganda imeendelea kuongoza kwa ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, ikiwa inashika nafasi ya 75 duniani – na Senegal inaendelea kuongoza kwa Afrika nzima ikiwa inashika nafasi ya 23 FIFA. 
  Katika 10 Bora mwezi huu Ujerumani bado inaongoza ikifuatiwa na Brazil, Ureno, Argentina, Ubelgiji, Hispania, Poland, Uswisi, Ufaransa na Chile.
  Sare ya 1-1 na wenyeji, Benin Novemba 12, mwaka huu katika mchezo wa kirafiki uliofanyika Uwanja wa l'Amitie, au Urafiki mjini Cotonou ilitarajiwa kuipandisha Tanzania, lakini bahati mbaya nchi imezidi kuporomoka.
  Katika mchezo huo uliochezeshwa na marefa wa nchini humo, Ligali Praphiou aliyesaidiwa na Bello Razack na Koutou Narcisse, bao la Benin lilifungwa na Nahodha wake, Stephane Sessegnon dakika ya 33 kwa penalti, kabla ya mshambuliaji Elias Maguri kuisawazishia Taifa Stars dakika ya 50 akimalizia krosi ya winga Shiza Kichuya kutoka upande wa kushoto.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: TANZANIA ‘MWENDO MDUNDO’ KUELEKEA CHINI, YAPOROMOKA TENA FIFA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top