• HABARI MPYA

  Jumapili, Desemba 31, 2017

  2017 ULIKUWA MWAKA WA TAMU NA CHUNGU KATIKA SOKA YETU

  SAA 6:00 usiku wa leo, nchi itapambwa na shamrashamra za kuuaga mwaka 2017 na kuukaribisha mwaka 2018.
  Ni siku ambayo wengine watabubujikwa na machozi kwa furaha za mafanikio zaidi, au kwa majonzi ya kupitia katika mwaka wa kumbukumbu za kuhuzunisha.
  Kati ya ambao wanauaga vibaya mwaka 2017 ni wapenzi wa soka nchini ambao kwa hakika wanaondoka katika mwaka wenye kumbukumbu za kuhuzunisha na kuumiza.

  MICHUANO YA KLABU AFRIKA
  Wawakilishi wetu kwenye michuano ya klabu barani, Azam na Yanga hawakuwa na safari ndefu baada ya kutolewa mapema tu katika Raundi ya kwanza.
  Yanga walifika Raundi ya Kwanza ya Ligi ya Mabingwa, baada ya kuitoa Ngaya Club ya Comoro kwa jumla ya mabao 6-2, wakishinda 5-1 ugenini na kupata sare ya 1-1 nyumbani, kabla ya kwenda kutolewa na Zanaco ya Zambia kwa bao la ugenini, baada ya sare ya 1–1 Dar es Salaam na sare ya 0–0 Lusaka.
  Kwa kutolewa kwenye hatua ya kuwania kuingia kwenye makundi, Yanga wakaangukia kwenye kapu la kuwania nafasi ya kucheza hatua ya makundi ya kombe la Shirikisho na huko nako bahati mbaya wakatolewa na MC Alger ya Algeria kwa jumla ya mabao 4-1, wakishinda 1–0 Dar es Salaam kabla ya kwenda kufungwa 4-0 Algeria.
  Azam FC wao walitolewa katika hatua ya kwanza tu, Raundi ya Kwanza tu ya Kombe la Shirikisho kwa jumla ya mabao 3-1 na Mbabane Swallows ya Swaziland, wakishinda 1–0 Dar es Salaam kabla ya kwenda kuchapwa 3-0 Mbabane.

  SERENGETI BORS:
  Timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Boys ikafanikiwa kufuzu fainali za Afrika nchini Gabon mwezi Mei baada ya ushindi wa rufaa yake dhidi ya Kongo Brazzaville kumtumia mchezaji aliyezidi umri, Langa Lesse Bercy.
  Na kwenye fainali hizo Sereneti Boys ilikaribia kukata tiketi ya fainali za Kombe la Dunia zilkizofanyika India kama si kuzidiwa mabao ya kufunga na Niger baada ya timu zote kulingana kwa pointi, nne kila moja.   

  TAIFA STARS:
  Nyota ya Tanzania ikaendelea kung’ara baada ya timu ya wakubwa, Taifa Stars kwenda kumaliza nafasi ya tatu kwenye michuano ya COSAFA nchini Afrika Kusini kufuatia kufungwa 4-2 na Zambia katika Nusu Fainali baada ya kuwatoa wenyeji, Bafana Bafana kwa kuwachapa 1-0 kwenye Robo Fainali.
  Lakini wakati wengi wakimaini michuano hiyo ingeisaidia Taifa Stars kufanya vizuri kwenye mechi za kufuzu CHAN, lakini ajabu ikaenda kutolewa Raundi ya kwanza tu ya mchujo kwa bao la ugenini na Rwanda, baada ya sare ya 1-1 Mwanza na sare ya 0-0 Kigali.
  Huo ulikuwa mwendelezo wa matokeo mabaya ya Taifa Stars katika michuano ya CAF baada ya kuanza vibaya katika mechi za Kundi L kufuzu fainali za Mataifa ya Afrika 2019 nchini Cameroon kufuatia kulazimishwa sare ya 1-1 na Lesotho Juni 10, Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
  Timu nyingine katika kundi hilo ni Uganda wanoongoza na Cape Verde wanaoshika mkia baada ya mechi za raundi ya kwanza tu. 
  Tanzania Bara ikahitimisha mwaka kwa kwenda kushika nafasi ya mwisho kwenye michuano ya CECAFA Challenge nchini Kenya, ambayo Zanzibar walifika fainali na kufungwa kwa penalti na wenyeji, Harambee Stars.

  MABADILIKO TFF
  Agosti mwaka huu, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) likapata uongozi mpya chini ya Rais Wallace Karia na Makamu wake, Michael Richard Wambura katika uchaguzi uliofanyika mjini Dodoma.
  Rais aliyemaliza muda wake, Jamal Malinzi hakugombea baada ya kuwekwa mahabusu kwa tuhuma za ubadhirifu na Karia, aliyekuwa Makamu Rais kwenye uongozi uliopita akajichukulia kiti kwa urahisi.
  Lakini baada ya miezi minne ya uongozi mpya, soka ya Tanzania imezidi kudidimia na kilelezo ni matokeo ya timu zetu kati ya Julai na sasa.

  SOKA YAHAMIA GEREZA LA KEKO
  Upepo mbaya ukaikumba soka ya Tanzania baada ya viongozi wote wa juu wa klabu kubwa, Simba na Yanga pamoja na TFF kuwekwa mahabusu gereza la Keko.
  Hao ni aliyekuwa Mwenyekiti wa Yanga, Yussuf Manji, Rais wa Simba, Evans Aveva na Makamu wake, Geoffrey Nyange ‘Kaburu’ pamoja na Rais wa TFF, Jamal Malinzi na Katibu wake, Selestine Mwesigwa.
  Manji alijiuzulu Uenyekiti wa Yanga mwezi Juni kutokana na kile alichosema sababu zilizo nje ya uwezo wake, ingawa tangu hapo kumekuwa na juhudi za wanachama kumbembeleza arejee.  
  Manji ambaye tayari ameachiwa na kufutiwa mashitaka, aliwekwa ndani kwa tuhuma za Uhujumu Uchumi, ikiwamo kukutwa na vitambaa vya sare za Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) akiwa amelazwa kitandani katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Dar es Salaam.
  Kwa yupande wake, Malinzi pamoja na Katibu wa TFF, Selestine Mwesigwa na Mhasibu, Nsiande Isawafo Mwanga walipelekwa rumande Keko Juni 29 baada ya kusomewa mashitaka 28 ya kughushi na kutakatisha fedha kupitia akaunti ya TFF iliyopo katika banki ya Stanbic, Dar es Salaam na tangu wameendelea kusota gereza la Keko.
  Katika mashitaka hayo, 25 yanakwenda moja kwa moja kwa Rais wa shirikisho hilo, Malinzi akidaiwa kughushi michakato mbalimbali ya kifedha, huku matatu yakiwahusu wote na Katibu wake na Mhasibu wake Nsiande Isawafo Mwanga.
  Nao Aveva na Makamu wake, Kaburu Juni 29, mwaka huu walipelekwa mahabusu hadi Julai 13, mwaka huu baada ya kunyimwa dhamana kufuatia kusomewa mashitaka matano Mahakama ya Hakimu Mkazi, Kisutu, Dar es Salaam na tangu hao wameendelea pia kusota gerezani.
  Wawili hao walifikishwa mahakamani mapema asubuhi ya siku hiyo na kusomewa mashitaka hayo matano mchana, ambayo ni pamoja na kughushi nyaraka zinazodai kuwa klabu ya Simba inawalipa madeni Rais Aveva na Makamu wake, Kaburu kiasi cha dola za Kimarekani 300,000.
  Makosa mengine ni Aveva kutoa nyaraka za uongo kwenye benki ya CRDB tawi la Azikiwe mjini Dar es Salaam Machi 10, 2016, la tatu ni kutakatisha fedha kinyume cha sharia, ambapo inadaiwa Rais huyo na Kaburu walikula njama za kufanya uhalifu huo.
  Shitaka la nne ni Kaburu kutakatisha fedha dola 300,000 na kuziweka kwenye benki ya  Barclays tawi la Mikocheni mjini Dar es Salaam, na la tano ni kutakatisha likimhusu tena, Makamu wa Rais, Kaburu aliyemsadia Aveva kutakatisha fedha katika Barclays baada ya kughushi nyaraka.

  MABADILIKO SIMBA, YANGA
  Hatimaye baada ya miaka zaidi ya 50 ya kuendeshwa katika mifumo isiyo na afya kwa ustawi wa klabu, Simba na Yanga zimeingia kwenye michakato rasmi ya mabadiliko ya mfumo ya kiundeshaji. 
  Simba walitangulia Desemba 3 baada ya Mohammed ‘Mo’ Dewji kushinda zabuni ya uwekezaji kwenye klabu hiyo, kufuatia kuwa mtu pekee aliweka dau la Sh Bilioni 20 kuomba asilimia 50 ya hisa, baada ya klabu kutangaza kuuza asilimia 50 ya hisa zake kwa Sh. Bilioni 20 Agosti.
  Hata hivyo, Serikali baadaye ikaagiza klabu hiyo isiuze zaidi ya asilimia 49 kwa mtu mmoja na Simba ikaahidi kutekeleza agizo hilo.
  Wiki iliyofuata tu, mahasimu wao wa jadi nao, Yanga wakaunda Kamati ya Kusimamia Mchakato wa Mabadiliko chini ya Mwenyekiti, mwanasheria maarufu nchini, Alex Mgongolwa na Makamu  Mwenyekiti, Profesa Mgongo Fimbo ambaye ni Mtaalam wa Katiba na Sheria za Ardhi.
  Wajumbe wa Kamati hiyo ni Mkuu wa zamani wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meckysadick, Mohamed Nyenge, ambaye ni Mchumi na Mwenyekiti wa Kamati ya Uchumi na Fedha, George Fumbuka ambaye ni  Mshauri wa Masuala ya Uwekezaji na Felix Mlaki ambaye ni Mchumi na Mtaalam wa Masuala ya Fedha.

  SOKA YA TANZANIA YAZIDI KUDIDIMIA
  SOKA ya Tanzania imezidi kudidimia baada ya kuporomoka kwa nafasi tano zaidi kwenye viwango vya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) kwa mwezi Novemba.
  Tanzania sasa inashika nafasi ya 147 kutoka ya 142 mwezi Oktoba, wakati Uganda imeendelea kuongoza kwa ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, ikiwa inashika nafasi ya 75 duniani – na Senegal inaendelea kuongoza kwa Afrika nzima ikiwa inashika nafasi ya 23 FIFA. 
  Na bahati mbaya zaidi Tanzania Bara, Kilimanjaro Stars ikafanya vibara kwenye michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Challenge – maana yake tutarajie taarifa mbaya zaidi mwanzoni mwa mwaka juu ya matokeo ya Desemba.

  KWAHERI 2017, KARIBU 2018
  Katika soka ni hayo tu mwaka 2017 klabu zetu hazikufanya vizuri kwenye michuano ya Afrika, Taifa Stars ikatolewa CHAN, ikaanza vibaya mechi za kufuzu AFCON 2019 kabla ya Kilimanjaro Stars kuhitimisha mwaka kwa kuboronga Challenge. Na hivyo ndivyo tunavyoaga mwaka 2017 na kuukaribisha mwaka 2018.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: 2017 ULIKUWA MWAKA WA TAMU NA CHUNGU KATIKA SOKA YETU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top