• HABARI MPYA

    Wednesday, December 20, 2017

    ALLIANCE ACADEMY WAPINGA USAJILI WA NG’ANZI SINGIDA UNITED

    Na Abdallah Chaus, MWANZA 
    KITUO cha kukuza na kuendeleza vipaji vya soka Tanzania, Alliance Academy cha mjini Mwanza kimepinga usajili wa kiungo Ally Khamis Ng’anzi kujiunga na Singida United.
    Ofisa wa Alliance Academy, Kessy Mziray ameiambia Bin Zubeiry Sports – Online leo kwamba wameandika barua Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kupinga usajili wa Ng’anzi aliyeibukia kwenye kikosi cha timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17 maarufu kama Serengeti Boys.
    Wiki iliyopita Singida United ilitaja wachezaji wapya iliyowasili akiwemo Ng’anzi aliyekuwemo kwenye kikosi cha Serengeti Boys kilichoshiriki fainali za Afrika nchini Gabon mwezi Mei mwaka huu.
    Ally Ng’anzi aliyeruka juu kupiga mpira kichwa wakati wa Mei mwaka huu nchini Gabon 

    Kessy ambaye pia kocha msaidizi wa Alliance FC inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara, amesema kwamba Ng’anzi ni mchezaji wao halali ambaye walimpokea kutoka katika mashindano ya Shule za Msingi yajulikanayo kama UMITASHUMITA mwaka 2011.
    “Na kwa usimamizi wa baba yake mzazi, huku alianza darasa la nne katika shule ya msingi ya Alliance na kufanikiwa kuhitimu darasa la saba na kufanikiwa kujiunga na kidato cha kwanza katika shule ya sekondari ya Alliance ya wavulana na kufika hadi kidato cha pili ndipo akaondoka kwenda timu ya taifa ya ya vijana chini ya umri wa miaka 15 na baadaye kupandishwa Serengeti Boys,”.
    Kessy amesema Ng’anzi na wenzake wawili, Cyprian Benedict na Israel Patrick Mwenda walikwenda kujiunga na Serengeti Boys kwa maelewano na TFF, lakini wenzake walirejea Mwanza mara baada ya mashindano kumalizika nchini Gabon.
    “Huku tukifanya jitihada za kumtafuta kwa kushirikiana na TFF tukafanikiwa kumpata katika kituo cha Cambianso kilichopo Dar es Salaam ambacho kilimsafirisha kwenda Tunisia kufanya majaribio katika klabu ya Etoile du Sahel, ambako hakufanikiwa na wakamrejesha Mwanza,”amesema Mziray.
    Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Singida United, Sanga Festo amesema kwamba wamemsaini mchezaji huyo kwa maelewano na kituo cha Cambianso, huku akiwashangaa Alliance kukimbilia katika vyombo vya Habari bila kuwasiliana nao.
    Mbali na Ng’anzi, Singida pia imewasajili wachezaji wengine waliokuwa Serengeti Boys ambao ni Issa Makamba, Mohammed Abdallah na Asad Juma.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: ALLIANCE ACADEMY WAPINGA USAJILI WA NG’ANZI SINGIDA UNITED Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top