• HABARI MPYA

    Friday, December 22, 2017

    MABINGWA SIMBA WASALIMISHA KOMBE MAPMEAAAA…WAPIGWA KWA MATUTA NA TIMU YA JESHI

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM 
    KIUNGO Jonas Gerald Mkude amegongesha mwamba penalti na Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ akamdakisha kipa zamani wa kimataifa nchini, Shaaban Dihile – Simba ikitolewa hatua ya 64 Bora, sawa na raundi ya Pili tu ya Kombe la Azam Sports Federation Cup (ASFC) leo.
    Maana yake, Simba SC imevuliwa ubingwa wa Azam Sports Federation baada ya kufungwa kwa penalti 4-3 kufuatia sare ya 1-1 ndani ya dakika 90 na timu ya Green Worriors ya Mwenge, inayomilikiwa na Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ).
    Katika mchezo huo uliofanyika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam kipa wa Simba, Aishi Manula alipangua penalti moja ya  Zuakuu Mgala kabla ya George Ossey kupiga nje, lakini penalti za Cecil Efram, Amir Hajji, Juma Mdingi na Idd Nyambi zilimpita.
    Wachezaji wa Simba wakiwa watulivu wakati wa kupiga penalti 
    Kiungo Muzamil Yassin (kushoto) akimtoka kiungo wa Green Warriors, Hassan Gumbo (kulia) 
    Beki wa Green Warriors, George Assey (kushoto) akimdhibiti mshambuliaji wa Simba, John Bocco
    Kiungo wa Simba, Said Ndemla akipasua katikati ya wachezaji wa Green Warriors
    Benchi timamu la Ufundi la Simba SC, kutoka kushoto Kocha Mkuu, Mcameroon Joseph Omog, Mrundi Masudi Juma na mzalendo, Muharammi Mohammed 'Shilton' leo Chamazi  

    Katika dakika 90 za mchezo huo, Green Warriors walitangulia kupata dakika ya 43 kupitia kwa mshambuliaji Hussein Bunu aliyefunga kwa kichwa akimalizia kazi nzuri ya Gido Chawala,
    Bao hilo lilidumu na hadi kipindi cha pili, ambako Simba walifanikiwa kusawazisha dakika ya 53 kwa penalti ya kiufundi ya Nahodha John Raphael Bocco ‘Adebayor’ baada ya Amiri Haji kuunawa mpira kwenye boksi katika harakati za kuokoa.
    Kutoka hapo, Simba walifunguka zaidi na kuanza kupeleka mashambulizi mfululizo langoni mwa Green Warriors, lakini sifa zimuendee kipa wa kikosi cha Taifa Stars kilichoshiriki CHAN mwaka 2009 nchini Ivory Coast, Shaaban Dihile aliyewaokoa michomo mingi ya hatari.
    Mwishoni mwa mchezo, refa mkongwe, Israel Nkongo alimuonyesha kadi ya njano Adam Said wa Green Warriors na kumtoa kwa kadi nyekundu. 
    Makocha wote wa Simba, Mcameroon Joseph Marius Omog na Msaidizi wake, Mrundi Masudi Juma na mzalendo, Muharammi Mohammed ‘Shilton’ ambaye ni kocha wa makipa walijadiliana vizuri wakati wa kuchagua wapiga penalti.
    Kocha wa Green Warriors, Azishi Kondo alikuwa mwenye furaha baada ya mechi kwa kuwatoa siyo tu mabingwa, bali pia timu yenye makocha wawili wa kigeni na wachezaji nyota na ghali.    
    Lakini kama walivyosema wahenga, Siku ya Kufa Nyani miti yote huteleza, pamoja na Aishi kuokoa penalti moja na Green Warriors kukosa moja, lakini haikusaidia Simba kusonga mbele na inatolewa mapema zaidi, tena na timu ya Daraja la Pili. 
    Kikosi cha Green Worriors kilikuwa; Shaaban Dihile, Edward William, Amir Hajji, Cecil Efram, George Ossey, Iddi Nyambi, Gido Chawala/Thomas Ndimbo dk63, Adam Said, Mohammed Athumani, Hussein Bunu na Hassan Gumbo/Juma Mdingi dk63.
    Simba SC; Aishi Manula, Erasto Nyoni, Ally Shomari/Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ dk67, Yusuph Mlipili, Juuko Murshid, Jonas Mkude, Shiza Kichuya, Muzamil Yassin, John Bocco, Said Ndemla na Mwinyi Kazimoto/Moses Kitandu dk50.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MABINGWA SIMBA WASALIMISHA KOMBE MAPMEAAAA…WAPIGWA KWA MATUTA NA TIMU YA JESHI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top