• HABARI MPYA

  Jumatano, Desemba 27, 2017

  YANGA SC KUIFUATA MBAO FC BILA CHIRWA

  Na Prince Akbar, DAR ES SALAAM
  YANGA SC itamkosa mshambuliaji wake Mzambia, Obrey Chirwa katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara Jumapili dhidi ya wenyeji, Mbao FC Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza.
  Yanga wanasema mchezaji huyo amekwenda kwao kwa sababu ya matatizo ya kifamilia, lakini habari nyingine zinasema mchezaji huyo amegoma kushinikiza alipwe madai yake.
  Chirwa ameposti picha kwenye akaunti yake ya Instagram akiwa ameshika jembe analima kwao Zambia, jambo ambalo limetafsiriwa kweli ana mgomo. 
  Mshambuliaji Mzambia, Obrey Chirwa hatasafiri na Yanga mjini Mwanza kwenye mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya wenyeji, Mbao FC Jumapili

  Kikosi cha kinaendelea na mazoezi mjini Dar es Salaam kabla ya safari ya Mwanza kesho au keshokutwa kwa ajili ya mchezo huo wa Ligi Kuu.
  Kwa ujumla Ligi Kuu inatarajiwa kuendelea Ijumaa baada ya mapumziko ya wiki tatu kupisha michuano ya CECAFA Challenge iliyomalizika nchini Kenya wiki iliyopita kwa wenyeji, Harambee Stars kuwa mabingwa wakiwafunga Zanzibar katika fainali.
  Ijumaa Azam FC watakuwa wenyeji wa Stand United Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam kuanzia Saa 1:00 usiku na Jumamosi kutakuwa na mechi tatu, Lipuli na Tanzania Prisons Uwanja wa Samora, Iringa kuanzia Saa 8:00 mchana, Mtibwa Sugar na Maji Maji Uwanja wa Manungu, Turiani, Morogoro na Ndanda FC na Simba SC Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara zote zikianza saa 10:00 jioni.
  Jumapili, mabingwa watetezi, Yanga watakuwa wageni wa Mbao FC Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza saa 10:00 jioni na Njombe Mji FC wataikaribisha Singida United kuanzia saa 8:00 mchana Uwanja wa Saba Saba, Njombe.
  Obrey Chirwa ameposti picha kwenye akaunti yake ya Instagram akiwa ameshika jembe analima kwao Zambia 
  Kwa picha hizo, imetafsiriwa kweli Obrey Chirwa ana mgomo Yanga

  Mechi za kukamilisha mzunguko wa 12 zitachezwa mwaka mpya, Januari 1 Mbeya City wakiikaribisha Kagera Sugar Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya  na Mwadui wakiikaribisha Ruvu Shooting zote kuanzia saa 10:00 jioni.
  Baada ya mechi hizo, Ligi Kuu itasimama tena kupisha mechi za Kombe la Mapinduzi visiwani Zanzibar na raundi ya tatu ya Azam Sports Federation Cup (ASFC) itakayochezwa kati ya Januari 5 na 7 mwakani kabla ya kuingia kwenye mzunguko wa 13 wa ligi kuanzia Januari 13 na 17, 2018.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: YANGA SC KUIFUATA MBAO FC BILA CHIRWA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top