• HABARI MPYA

  Jumamosi, Desemba 30, 2017

  SIMBA RAHA TUPU, YAIPIGA NDANDA 2-0 NA KURUDI KILELENI LIGI KUU

  Na Mwandishi Wetu, MTWARA
  SIMBA SC imerejea kileleni mwa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara baada ya ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya wenyeji, Ndanda FC jioni ya leo Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara.
  Shujaa wa Simba leo alikuwa ni mshambuliaji na Nahodha wa sasa, John Raphael Bocco aliyefunga mabao yote hayo kipindi cha pili baada ya dakika 45 ngumu za kipindi cha kwanza.
  Kwa ushindi huo, Simba inafikisha pointi 26 baada ya kucheza mechi 12, sawa na Azam FC walio nafasi ya pili kwa kuzidiwa wastani wa mabao.
  Mabingwa watetezi Yanga SC wenye pointi 21 wanaendelea kushika nafasi ya tatu na wataendelea kukaa hapo hata wakishinda kesho dhidi ya Mbao FC mjini Mwanza sana washuke tu kama watatoa sare au kupoteza na Singida United washinde ugenini dhidi ya Njombe Mji FC.
  Katika mchezo wa leo Uwanja wa Nangwanda, Bocco alifunga bao la kwanza kwa kichwa dakika ya 52 akimalizia kona nzuri ya winga Shiza Kichuya kutoka upande wa kulia.
  Bocco, mchezaji wa zamani wa Azam FC akafunga bao la pili dakika ya 56 akitumia makosa ya mabeki wa Ndanda na kipa wao, Jeremiah Kisubi kuzembea kuokoa mpira mrefu ulioingizwa kwenye eneo lao la hatari.
  Ndanda walijitahidi kuendelea kupeleka mpira kwenye eneo la Simba, wakiongozwa na mkongwe Mrisho Khalfan Ngassa, lakini umaliziaji mbovu ukawakosesha japo la kufutia machozi.
  Katika mchezo uliotangulia mchana wa leo, bao pekee la Salum Kimenya liliipa ushindi wa 1-0 Tanzania Prisons dhidi ya wenyeji, Lipuli FC Uwanja wa Samora mjini Iringa.
  Mechi nyingine ya Ligi Kuu leo, Mtibwa Sugar wameshinda 2-1 dhidi ya Maji Maji Uwanja wa Manungu, Turinia, Morogoro. Mabao ya Mtibwa yamefungwa na Hassan Dilunga dakika ya 13 na Riffat Khamis dakika ya 66  baada ya Jaffar Mohamed kutangulia kuifungia Maji Maji dakika ya tisa.     
  Kikosi cha Ndanda FC kilikuwa; Jeremiah Kisubi, William Lucian, Abdallah Suleiman/Ayoub Masoud dk51, Ibrahim Job, Hamad Waziri, Hemed Khoja/Omar Mponda dk61, Jacob Massawe, Majid Khamis, John Tibar/Alex Sethi dk72, Jabir Aziz na Mrisho Ngassa. 
  Simba SC; Aishi Manula, Paul Bukaba, Shiza Kichuya, Juuko Murshid, Erasto Nyoni, Jonas Mkude, John Bocco, James Kotei/yussuf mlipili dk72, Juma Luizio/Moses KItandu dk54, Muzamil Yassin na Mohamed Ibrahim ‘Mo’/Said Ndemla dk38.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: SIMBA RAHA TUPU, YAIPIGA NDANDA 2-0 NA KURUDI KILELENI LIGI KUU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top