• HABARI MPYA

  Ijumaa, Desemba 29, 2017

  YANGA WAINGIA MWANZA KWA KISHINDO KUIZIMA MBAO FC

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  KAIMU Mwenyekiti wa Yanga, Clement Sanga ameongoza msafara wa watu 30 wa klabu hiyo uliotua jijini Mwanza leo kuikabili Mbao FC Jumapili katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara Uwanja wa CCM Kirumba.
  Akizungumza na Waandishi wa Habari makao makuu ya klabu, Jangwani, Dar es Salaam leo, Msafara huo wa kikosi cha Yanga unajumuisha wachezaji 21, maofisa wa benchi la ufundi pamoja na viongozi wa klabu hiyo.
  "Timu imeshafika salama Mwanza na leo jioni itafanya mazoezi kwenye uwanja wa Alliance na kesho itakuwepo kwenye uwanja wa CCM Kirumba ambao utachezewa hiyo mechi," alisema Katibu Mkuu wa Yanga, Boniface Mkwasa.
  Ikumbukwe Yanga SC ilifungwa na Mbao FC 1-0 mechi zote mbili za msimu uliopita mjini Mwanza, kwanza katika michuano ya Azam Sports Federation Cup (ASFC) Aprili 30 na baadaye katika Ligi Kuu Mei 20 baada ya mabingwa hao wa Ligi Kuu kushinda 3-0 kwenye mchezo wa kwanza wa ligi Oktoba 29, mwaka 2016 Dar es Salaam.
  Wachezaji wa Yanga wakiwa kwenye ndege leo kwa safari ya Mwanza kwa ajili ya mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya wenyeji, Mbao FC Jumapili

  Mkwasa katika hatua nyingine amewanyooshea kidole baadhi ya watendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilala kwa uzembe unaozorotesha ukarabati wa Uwanja wa Kaunda.
  "Zoezi letu la kujaza kifusi kwenye uwanja wa Kaunda linaendelea lakini nijaribu kuelezea masikitiko yetu kutokana na kuwepo kwa mtaro unaotiririsha maji machafu kwenye uwanja wetu hali iliyopelekea ukuta kubomoka.
  Tumejaribu kuonana na baadhi ya wahusika kwenye Manispaa lakini wamekuwa hawatupi ushirikiano. Tunawaomba huo mtaro uendelezwe ukamwage hayo maji hayo machafu sehemu ambako ulitakiwa kuishia ikishindikana tutalifikisha hili kwenye vyombo vya kisheria," alisema Mkwasa.
  Katibu Mkuu wa Yanga, Charles Boniface Mkwasa (kulia) akizungumza na Waandishi wa Habari leo makao makuu ya klabu, Jangwani, Dar es Salaam. Kushoti ni Ofisa Habari, Dismas Ten 

  Katika hatua nyingine Afisa Habari wa Yanga, Dismas Ten alisema klabu hiyo imepania kutwaa ubingwa wa kombe la Mapinduzi.
  "Tukimaliza mechi yetu na Mbao, kikosi chetu kitaelekea moja kwa moja Visiwani Zanzibar ambako tutashiriki mashindano hayo.
  Sisi Yanga ni klabu ya kushinda hivyo tutakwenda na kikosi kamili tukiwa na lengo la kutwaa ubingwa," alisema Ten.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: YANGA WAINGIA MWANZA KWA KISHINDO KUIZIMA MBAO FC Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top