• HABARI MPYA

  Jumatano, Desemba 27, 2017

  WEAH ATANGAZWA RASMI KUWA RAIS MPYA LIBERIA

  MWANASOKA bora wa zamani wa Dunia, George Weah ametangazwa rasmi kuwa Rais mpya wa nchi yake, Liberia.
  Mchezaji huyo wa zamani wa Monaco ya Ufaransa, George Weah mwenye umri wa miaka 51, ameshinda Urais wa Liberia baada ya kushinda majimbo 12 kati ya 15 ya nchi hiyo ya Magharibi mwa Afrika.
  Mpinzani wake mwenye umri wa miaka 73 na Makamu wa Rais wa sasa, Joseph Boakai amepata majimbo mawili tu.
  Mwafrika huyo pekee kushinda Ballon d’Or, Weah aliyeweika pia AC Milan, Paris Saint-Germain, Marseille za Ufaransa, AC Milan, Chelsea na Manchester City, ameandika kwenye ukurasa wake wa Twitter kuwashukuru mashabiki akisema amepanga kuleta mapinduzi katika nchi hiyo.
  Kwa ushindi huo, mshambuliaji huyo aliyegeukia siasa anakuwa rais wa 25 wa nchi hiyo.
  Weah aliyezaliwa Oktoba 1 mwaka 1966 ni mmoja kati ya wanasoka bora zaidi kuwhai kutokea Afrika. Ndiye Mwafrika pekee kuwahi kutwaa tuzo ya Mwanasoka Bora wa Dunia mwaka 1995. Amekuwa Mwanasoka Bora wa Afrika katika miaka ya 1989, 1994 na 1995. Mwaka 2004 alitajwa kwenye orodha ya wanasoka 100 babu kubwa duniani walio hai.
  Weah alicheza kwa miaka 14 Ulaya katika nchi za Ufaransa, Italia na England na ni kocha wa sasa wa Arsenal, Arsene Wenger aliyempeleka Ulaya akimsajili Monaco mwaka 1988 kabla ya kuhamia Paris Saint Germain mwaka 1992 ambako alishinda mataji ya Ligue 1 mwaka 1994 na kuibuka mfungaji bora wa Ligi ya Mabingwa msimu wa 1994–1995. 
  Akasajiliwa na A.C. Milan mwaka 1995 ambako alikuwa na misimu minne mizuri mno, akifunga mabao muhimu la kukumbukwa zaidi ni dhidi ya Verona, na akashinda mataji mawili ya Serie A. Akahamia Ligi Kuu ya England kumalizia soka yake ambako alicheza Chelsea na Manchester City.
  Baada ya kustaafu soka, Weah amehamia kwenye siasa na aligombea Urais wa Liberia kwa mara ya kwanza mwaka 2005 akashindwa na Ellen Johnson Sirleaf katika kura za marudio. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: WEAH ATANGAZWA RASMI KUWA RAIS MPYA LIBERIA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top