• HABARI MPYA

  Jumanne, Desemba 26, 2017

  SIMBA SC YAINGIA KAMBINI LEO KUJIANDAA NA NDANDA

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  SIMBA SC inaingia kambini leo mjini Dar es Salaam kwa maandalizi ya mchezo wake ujao wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya Ndanda FC Desemba 30, mwaka huu Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara.
  Kocha Mrundi, Masudi Juma akisaidiwa na kocha wa makipa Muharami Mohammed ‘Shilton’ wataiongoza timu kuanzia leo kufuatia kuondolewa kwa aliyekuwa kocha mkuu, Mcameroon, Joseph Marius Omog.
  Omog alifukuzwa Jumamosi, siku moja tu baada ya Simba kuvuliwa ubingwa wa michuano ya Azam Sports Federation (ASFC) katika hatua ya 64 Bora baada ya kufungwa kwa penalti 4-3 kufuatia sare ya 1-1 ndani ya dakika 90 na timu ya Green Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
  Wachezaji wa Simba SC wanaingia kambini leo mjini Dar es Salaam kujiandaaa na mchezo dhidi ya Ndanda FC Desemba 30 

  Kwa ujumla Ligi Kuu inarejea wikiendi hii baada ya kusimama kwa wiki tatu kupisha michuano ya CECAFA Challenge nchini Kenya iliyomalizika wiki iliyopita kwa wenyeji kubeba taji wakiishinda Zanzibar katika fainali kwa matuta baada ya sare ya 2-2 ndani ya dakika 120. 
  Ijumaa Azam FC watakuwa wenyeji wa Stand United Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam kuanzia Saa 1:00 usiku na Jumamosi kutakuwa na mechi tatu, Lipuli na Tanzania Prisons Uwanja wa Samora, Iringa kuanzia Saa 8:00 mchana, Mtibwa Sugar na Maji Maji Uwanja wa Manungu, Turiani, Morogoro na Ndanda na Simba, zote saa 10:00 jioni.
  Jumapili, mabingwa watetezi, Yanga watakuwa wageni wa Mbao FC Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza saa 10:00 jioni na Njombe Mji FC wataikaribisha Singida United kuanzia saa 8:00 mchana Uwanja wa Saba Saba, Njombe.
  Mechi za kukamilisha mzunguko wa 12 zitachezwa mwaka mpya, Januari 1 Mbeya City wakiikaribisha Kagera Sugar Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya  na Mwadui wakiikaribisha Ruvu Shooting zote kuanzia saa 10:00 jioni.
  Baada ya mechi hizo, Ligi Kuu itasimama tena kupisha mechi za Kombe la Mapinduzi visiwani Zanzibar na raundi ya tatu ya Azam Sports Federation Cup (ASFC) itakayochezwa kati ya Januari 5 na 7 mwakani kabla ya kuingia kwenye mzunguko wa 13 wa ligi kuanzia Januari 13 na 17, 2018.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: SIMBA SC YAINGIA KAMBINI LEO KUJIANDAA NA NDANDA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top