• HABARI MPYA

    Monday, December 25, 2017

    SABA ZA ‘MCHANGANI’ ZAFUZU 32 BORA KOMBE LA AZAM SPORTS FEDERATION

    Na Paschal Kabombe, DAR ES SALAAM
    TIMU 12 za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, 11 za Daraja la Kwanza, tatu za Daraja la Pili na nne za Ligi ya Mabingwa wa Mikoa zimefuzu hatua ya 32 ya michuano ya Azam Sports Federation Cup (ASFC).  
    Kamati ya Mashindano ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) inasubiriwa kutoa maamuzi juu ya mechi mbili kati ya Abajalo ya Daraja la Kwanza dhidi ya Tanzania Prisons na  Mvuvumwa (Daraja la Kwanza) na JKT Ruvu Ligi Kuu ambazo hazikufanyika katika hatua ya 64 Bora kutokana na baadhi ya wachezaji kukosa leseni.
    Na hiyo ilitokana na mfumo wa usajili kwa njia ya mtandao wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) unaojulikana kama TMS kufeli hali iliyosababisha klabu kushindwa kukamilisha usajili kwa wakati kupitia mfumo huo.
    Green Warriors ya Daraja la Pili imewatoa waliokuwa mabingwa watetezi, Simba SC 

    TFF iliagiza klabu ziwasilishe moja kwa moja usajili wake makao makuu ya shirikisho, Uwanja wa Karume, Dar es Salaam, ingawa siku moja kabla ya kuanza mechi za hatua ya 64 Bora ASFC mfumo huo ulifunguliwa tena baada ya marekebisho ya hitilafu zilizojitokeza kufuatia shirikisho hilo kuwasiliana na waendeshaji wa mfumo huo  walioko Tunis, Tunisia na klabu zikatakiwa kuendelea kusajili hadi Desemba 23 dirisha lilipofungwa tena.
    Timu za Ligi ya Mabingwa wa mikoa zilizofuzu ni Buseresere FC ya Geita, Majimaji Rangers ya Nachingwea, Lindi, Kariakoo United ya Lindi Mjini na Shupavu FC ya Morogoro, wakati za Daraja la Pili ni Green Warriors ya Dar es Salaam iliyowatoa mabingwa watetezi, Simba, Ihefu FC ya Mbeya iliyoitoa Mbeya City na Burkina Faso FC ya Morogoro iliyoitoa Lipuli ya Iringa. 
    Timu za Daraja La Kwanza  ni Toto Africans ya Mwanza, KMC, Polisi, Friends Rangers za Dar es Salaam, Polisi Tanzania ya Morogoro, Rhino Rangers ya Tabora, JKT Oljoro ya Arusha, Biashara United ya Mara, Pamba SC ya Mwanza, Kiluvya United ya Pwani na Dodoma FC ya Dodoma. 
    Timu za Ligi Kuu ni pamoja na makamu bingwa, Mbao FC ya Mwanza, Ndanda FC ya Mtwara, Njombe Mji ya Njombe, Kagera Sugar ya Bukoba, Stand United ya Shinyanga, Singida United ya Singida, Ruvu Shooting ya Pwani, Mwadui FC ya Shinyanga, Maji Maji FC ya Songea, Azam FC, Yanga SC za Dar es Salaam na Mtibwa Sugar ya Morogoro.
    Droo ya hatua ya 32 Bora inatarajiwa kupangwa wiki ijayo ‘live’ katika studio za Azam TV, Tabata mjini Dar es Salaam. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SABA ZA ‘MCHANGANI’ ZAFUZU 32 BORA KOMBE LA AZAM SPORTS FEDERATION Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top