• HABARI MPYA

  Saturday, September 16, 2017

  YANGA WAPANIA KUBEBA POINTI TATU SONGEA LEO

  Na Mwandishi Wetu, SONGEA
  MABINGWA watetezi, Yanga SC leo wanatarajiwa kucheza mechi ya pili mfululizo Nyanda za Juu Kusini watakapoteremka Uwanja wa Maji Maji mjini Songea, kumenyana na wenyeji, Maji Maji katika mfululizo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania.
  Yanga inacheza Songea leo, ikitoka kushinda 1-0 katika mchezo wake mwingine wa Nyanda za Juu Kusini dhidi ya wenyeji, Njombe Mji FC Jumapili iliyopita Uwanja wa Saba Saba na leo kocha Mzambia, George Lwandamina anataka kuendeleza wimbi kla ushindi.
  Safu ya ulinzi ya Yanga leo itakutana na washambuliaji wake wake wawili wa zamani Jerson John Tegete na Danny Mrwanda ambao kwa sasa wanaiongoza Maji Maji.
  Msimu uliopita Yanga ilivuna pointi zote sita kwa Maji Maji kwa ushindi wa nyumbani na ugenini, lakini kihistoria mechi za Songea huwa ni ngumu kwa Yanga hata iwe na kikosi bora kiasi gani. 
  Mechi nyingine za Ligi Kuu leo, Mbao watakuwa wageni wa Mtibwa Sugar Uwanja wa Manungu, Turiani mkoani Morogoro, Tanzania Prisons watakuwa wenyeji wa Ndanda FC saa 10: 00 jioni kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya, Lipuli FC watakuwa wenyeji wa Ruvu Shooting Uwanja wa Samora, Iringa wakati Stand United wataikaribisha Singida United Uwanja wa Kambarage, Shinyanga.
  Ligi Kuu itaendelea tena kesho Uwanja wa Sokoine, Mbeya City wakiikaribisha Njombe Mji na Uwanja wa Uhuru, Simba SC wakiikaribisha Mwadui FC ya Shinyanga mechi zote zikianza Saa 10: 00 jioni.
  Wakati huo huo: Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara nayo inatarajiwa kuanza leo, Kundi A Mgambo wakiikaribisha JKT Ruvu katika Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga wakati Kundi B Mawenzi Market watakuwa wenyeji wa KMC ya Kinondoni, kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro na Mufindi United watakuwa wageni wa Polisi Dar Uwanja wa Azam, Chamazi, Dar es Salaam.
  Kundi C: kutakuwa na mchezo mmoja kwa siku ya Jumamosi ambako Rhino ya Tabora itakuwa mwenyeji wa Alliance Schools kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: YANGA WAPANIA KUBEBA POINTI TATU SONGEA LEO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top